Rais Samia alipa makavu Jeshi la Polisi

HomeKitaifa

Rais Samia alipa makavu Jeshi la Polisi

Ni juzi tu tangu alipotoa maagizo ya kurekebisha utendaji wa Jeshi  la  Magereza nchini, Rais Samia Suluhu Hassan jana ameligeukia Jeshi la Polisi na kulitaka  kufanya mageuzi makubwa ndani ya jeshi hilo ikiwemo kuhakikisha matumizi mazuri ya fedha.

Rais Samia aliyekuwa akifungua Kikao Kazi cha Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, Makamanda wa Polisi wa Mikoa  na Vikosi jana Agosti 30, 2022 mkoani Kilimanjaro amesema pamoja na hatua zilizoanza kuchukuliwa, mageuzi makubwa yanatakiwa hususani ya  kiutawala na kiufundi ndani ya jeshi hilo.

“Naomba mniruhusu mimi  niingie kwa undani zaidi kulitathmini Jeshi la Polisi halafu tuone namna tunavyoenda kujirekebisha,” amesema Rais Samia wakati akianza hutuba yake.

Kutokana na kuwepo kwa baadhi ya mambo ambayo yamelitia doa Jeshi la Polisi Tanzania ikiwemo baadhi ya askari kushiriki katika vitendo vya uvunjaji wa  sheria na haki za binadamu ,ubadhirifu na kufanya vitendo visivyo vya kimaadili, Rais Samia ameagiza yafuatayo ili yasijitokeze tena:

Kuboresha uongozi na uendeshaji wa Jeshi

Rais Samia amesema kutokana na kutokuwa na  mahusiano mazuri kati ya Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani, Jeshi la Polisi limekuwa na matumizi mabaya ya fedha za bajeti, hivyo amelitaka jeshi kuimarisha mahusiano na wizara.

Katika muktadha wa  kuimarisha mahusiano kati ya jeshi na wizara,  Rais Samia amekemea tabia ya baadhi ya makamanda wa jeshi hilo kutoheshimu viongozi wa wizara na kufanya mawasiliano moja kwa moja na viongozi wa juu.

‘Wizara na jeshi muwe karibu sana katika utendaji nitakachomuuliza  IJP (Inspekta Jenerali wa Polisi) ndicho hicho anijibu waziri kukiwa na jawabu tofauti ina maana hamko vizuri,” amesema Rais.

Kugeukia Matumizi ya Tehama

Kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ulimwenguni Rais Samia amelitaka jeshi hilo kutumia Tehama katika utendaji kazi ili kuendana na nyakati  kwani wahalifu hubuni mbinu mpya kila uchao.

Rais amesema Serikali inaangalia namna itakavyowezesha suala hilo kwa haraka hata katika mafunzo ya askari ili kuimarisha utendaji.

Matumizi sahihi ya fedha na mafuta

Licha ya Jeshi la Polisi kutotumia vema fedha za bajeti ya Serikali  imeelezwa kuwa kumekuwa na matumizi yasiyo sahihi ya fedha wanazokatwa askari wa Jeshi la Polisi katika mishahara yao pamoja na uwepo wa miradi isiyoakisi kiwango halisi cha fedha.

Kutokana na hilo Rais ameagiza kuwepo na nidhamu ya fedha ndani ya Jeshi hilo na kutumia fedha  katika malengo yaliyokusudiwa.

“Kama mfuko unaitwa kufa na kuzikana watu wakatwe, wanapofiwa pesa itoke lakini pesa inakatwa,baskari wanafiwa hawafaidiki, wanaofaidika ni wachache lakini ukienda kutazama fedha walizochanga hazipo,” amesema Samia.

Aidha, Rais Samia amekemea  tabia ya baadhi ya maaskari kutumia mafuta ya magari yanayotolewa na Serikali kwa makamanda wa mikoa na wilaya kwa shughuli zao binafsi ikiwemo magari ya biashara.

Kuimarisha mafunzo kwa maaskari

Kwa mujibu wa Rais Samia tathmini imeonesha kuwa utendaji kazi usio wa kuridhisha wa Jeshi la Polisi katika baadhi ya maeneo pamoja na mmomonyoko wa maadili kwa askari umechangiwa na kutokuwepo kwa mafunzo.

Amelitaka jeshi hilo kufanyia kazi mitaala pamoja na kuboresha vitendea kazi vya mafunzo ya kimedani na ya darasani ambapo tayari Serikali imetoa Sh11 bilioni kwa ajili ya mafunzo.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiagana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camilius Wambura pamoja na Makamanda wengine wa Jeshi hilo mara baada ya kufungua Kikao Kazi cha Makamanda hao.

Kuacha rushwa, muhali na uzembe

Rais Samia amesema mambo hayo matatu ndiyo yanayochangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa makosa ya uhalifu na hiyo imesababisha kuundwa kwa tume inayolitathmini Jeshi la Polisi ili kuboresha utendaji kazi wake.

Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23 imetenga kiasi cha Sh50 bilioni kwa ajili ya posho na mishahara ya askari hivyo amemtaka IJP kuhakikisha fedha hizo zinafika kwa askari wote ili kuwapa morali ya kufanya kazi kwa weledi.

Pamoja na mambo mengine Rais Samia amelitaka Jeshi la Polisi kuboresha utendaji kazi wake visiwani Zanzibar kwani ni sehemu muhimu na ya kimkakati hivyo inaweza kutumiwa na wahalifu kufanya vitendo viovu.

Itakumbukwa huu ni mkutano wa kwanza kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IJP) Camillus Wambura  kufanya na Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Vikosi tangu  alipoteuliwa na kuapishwa na Rais mnamo Julai 20 mwaka huu akichukua nafasi ya Simon Sirro aliyeteuliwa kuwa balozi nchini Zimbabwe.

Awali  IJP Wambura amesema jeshi hilo tayari lina  mikakati ya kukabiliana na uhalifu ikiwemo kuongeza ushirikiano na mataifa jirani pamoja na raia pia kutoa mafunzo kwa askari ili kuwaweka katika hali ya ukakamavu na utayari muda wote.

Wambura amesema katika kukabiliana na wimbi la ajali za barabarani wanaendelea kutoa elimu ya usalama barabarani, kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaokiuka pamoja na kuwaagiza makamanda wa mikoa kusimamia vikosi vya usalama barabarani ipasavyo.

“Nimewaagiza makamanda wote kusimamia askari wa kikosi cha usalama barabarani na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo na wasisite kuchukua maadili kwa wale watakaokiuka maadili ya kazi zao na watakao onesha muhali wataondolewa kwenye nafasi zao na kuchukuliwa hatua zaidi,” amesema Wambura.

error: Content is protected !!