Rais Samia ameandika historia Uwanja wa Kimataifa

HomeKimataifa

Rais Samia ameandika historia Uwanja wa Kimataifa

Na Dk Juma Mohammed, Zanzibar

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya ziara rasmi  katika Jamhuri ya Watu wa China. 

Rais Samia amealikwa rasmi na Rais wa China, Xi Jimping.

Rais Samia anakuwa Mkuu wa Nchi na Serikali wa kwanza kualikwa na Rais Xi Jimping baada ya kiongozi huyu kuchaguliwa tena kuwa Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China.

Rais Samia ameandika histioria ya pili katika Uhusiano wa Tanzania –China baada ile ya Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.  

Itakumbukwa kuwa Mwaka 2013 Rais wa China alifanya ziara yake ya kwanza nje ya Taifa hilo hapa Tanzania mara tu baada ya kushika wadhifa wa Urais na Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya CCP. 

Baadhi mtauliza ameandika historia ipi?

Jibu ni kwamba Rais Samia kama nilivyoeleza awali amekuwa Mkuu wa Nchi na Serikali wa kwanza kualikwa na Rais Xi Jimping mara tu baada ya Kiongozi huyo kumaliza Mkutano Mkuu wa Chama chake na kuchaguliwa tena kuongoza Taifa hilo.

Ni muhimu kuelewa kuwa hadi mtu anafikia kukualika nyumbani kwake basi huyo mtu atakuwa amekukinai vya kutosha. Mtu mashaka mashaka tu huwezi kualikwa.

Hii ni heshima kubwa kwetu Watanzania kwa kuwa na Kiongozi makini na anayekubalika ndani na katika uwanja mpana wa Kimataifa.

Uhusiano wa nchi mbili hizi ulianza mwaka 1964 baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lakini ikumbukwe kuwa China ilikuwa nchi ya mwanzo kuyatambua Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoongozwa na Chama cha ASP.

Niweke wazi kuwa, Rais Xi Jimping ni mmoja kati ya Marais wenye nguvu katika Ulimwengu wa leo, Taifa lake ni la pili kwa uchumi imara na uchumi mkubwa.

Kitendo cha Rais huyo mwenye nguvu za Kiuchumi na Kijeshi kumualika Rais Samia kukanyaga ardhi ya Uchina mara tu baada ya kutoka kuaminiwa tena na Wachina kuongoza CCP na Taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu ni dhahiri kuwa Rais Samia ameseti “New World Order.

Rais Samia amekuwa Mkuu wa nchi wa mwanzo kutua katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Beijing na kukanyaga ardhi ya Uchina tangu mwaka 2019 mara ya mwisho viongozi wa Kitaifa kutoka Mataifa mbalimbali kutembelea China.

Miaka 73 iliyopita, China ilikuwa taabani kabisa baada ya Vita ya Pili ya Dunia, Lakini chini ya uongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China, sasa China imekuwa nchi ya pili kwa ukubwa wa kiuchumi duniani na pato la taifa limeongezeka mfululizo kwa kiwango cha juu.

Jamhuri ya Watu wa China imemaliza mchakato wa uchumi wa viwanda uliohitaji miaka mingi katika nchi za magharibi. 

Ikiwa ni  miaka 73 sasa tangu kuundwa kwa Jamhuri ya Watu wa China chini ya Chama cha CCP, wananchi wa China wameshikamana kutatua changamoto mbalimbali katika njia ya ujamaa wenye sifa za kichina.

China imefuata kanuni tano za kuishi pamoja kwa Amani na kushirikiana na watu wa nchi zote za dunia ili kujenga mustakabali mzuri wa pamoja wa binadamu. 

Jamhuri ya Watu wa China imepiga hatua kubwa za kujitegemea, kujistawisha na kujiimarisha.

China ilianza kufanya mageuzi katika uchumi mwaka 1978 kwa kufungua milango,lakini pia ikifuatilia kwa umakini sana utekelezaji wa siasa ya mageuzi. 

Mwaka 2018, Pato la Taifa la China limefikia dola za kimarekani trilioni 13.6, kiasi ambacho ni mara 175 ikilinganishwa na ilivyokuwa  mwaka 1949.

Kiasi hicho kinachukua 16% ya jumla ya dunia. 

Hali kadhalika, watu maskini nchini China wamepungua milioni 740. 

China ikawa nchi ya kwanza iliyofikia lengo la kupunguza umasikini la Umoja wa Mataifa ikichangia zaidi ya asilimia 70 ya upunguaji wa maskini duniani.

Kuna umuhimu na ulazima wa kipekee kumuweka katika shajara ya kihistoria Rais Samia kukubalika kwake na Taifa kubwa lenye uchumi mkubwa la Jamhuri ya Watu wa China na Mataifa mengine.

Lazima tujivunie kuwa na Mkuu wa Nchi na Serikali, Rais Samia ambaye viongozi wenzake wa Mataifa makubwa kama China wanaona fakhari na umuhimu wa kumualika katika kukuza uhusiano wa Mataifa haya.

Rais Xi Jimping ni Rais mtulivu, mpole, mchapakazi kama ilivyo kwa Rais wetu Samia nae ni mtulivu, mpole, mchapakazi na ambaye hana papara,lakini pia ni mwenye huruma, hekma na busara.

Rais Samia ameiweka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uwanja mpana zaidi wa kimataifa kwa kukuza ushirikiano wa Jumuiya za Kimataifa, Kikanda na kuimarisha uhusiano wa nchi na nchi  miongoni mwa nchi marafiki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan China.

Wachina wanamsemo wao wanasema “Watanzania ni ndugu zetu wa damu” hakika kabisa msemo huo unathibitishwa na Mualiko wa Rais Xi Jimping kwa Rais Samia.

Huu ni mwaka wa 58 tangu Tanzania na China zianzishe uhusiano wa kibalozi.

Urafiki wetu uliojengwa na waasisi wa mataifa Mwalimu Julius K. Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong umekuwa tunu inayothaminiwa na wananchi wote wa nchi mbili. 

Katika miaka 58 iliyopita, Tanzania na China zimekuwa zikiaminiana kisiasa, kushirikiana kwa ufanisi mkubwa na kuwasiliana mara kwa mara.

Katika hotuba yake huko Beijing, Rais Xi Jinping alitangaza mwongozo wa uaminifu wa hali ya juu, ushirikiano wa kweli, urafiki wa dhati pamoja na dhana sahihi ya haki na maslahi nchini Tanzania.

Juhudi kubwa amezichukua Rais Samia katika kuweka sawa Diplomasia yetu katika Jumuiya ya Kimataifa. 

Rais Samia ameiweka Tanzania peupeni katika Jumuiya ya Kimataifa.

Sasa hatusemi tena kwenye vibuyu,tunasema na wanatusikiliza tena katika mikutano au vikao vinavyowakutanisha Viongozi wa kimataifa,Wakuu wa Mashirika makubwa ya kimataifa,matajiri wa Ulimwengu.

Kutokana na kazi kubwa inayoendelea kufanywa na Rais Samia, wengi katika matajiri wa Dunia na mashirika makubwa ya kimataifa wanashauku ya kuwekeza Tanzania.

 

error: Content is protected !!