Serikali imepunguza gharama za leseni kwa maofisa usafirisha wa bodaboda, bajaji na guta zinazotumia umeme katika bajeti ya mwaka 2025-2026 kulipia kiasi cha Sh 30,000.
Hatua hiyo imedhihirisha usikivu wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wake hususani maofisa usafirishaji.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo wakati wa ufungaji wa mafunzo kwa madereva guta za umeme yaliyofanyika katika chuo cha Polisi ikiwa ni mwezi mmoja toka atangaze maofisa hao wanahakikisha wanasajiliwa.
Akizungumza na madereva hao, wakufunzi na viongozi wa shirikisho la maafisa hao Mpogolo amesema usikivu wa Rais Samia umeendelea kuhakikisha vilio vya madereva wa vyombo vya moto vinasikilizwa na kupatiwa ufumbuzi ili waweze kufanya shughuli zao kwa amani.
Ameeleza kuwa kutolewa kwa mafunzo hayo na jeshi la polisi kutasaidia kuongeza uelewa na usalama, kutambulika rasmi kama familia kwa kusajiliwa tofauti na awali hawakuwa na leseni na hawakujulikana kwa urahisi.