Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewasihi wananchi kushiriki kikamilifu kwenye chaguzi za Serikali za Mitaa ili waweze kupata viongozi wazuri wanaowafaa.
Amesema hayo katika Ibada ya kumsimika kazini Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Azania Front jijini Dar es Saalam.
“Natoa wito kwa wananchi kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kwa vyama vya siasa viteue wagombea wazuri ili wananchi wawe na uwanja mpana wa kuchagua viongozi wazuri wanaowafaa.”- amesema Rais Samia.
Rais Samia pia amesema pia kuwa ahadi ya Serikali ni kuendelea kutunza amani nchini kwani ndio kichocheo kikubwa cha maendeleo na ustawi wa nchi.
“Serikali itaendelea kutunza amani ya nchi yetu ili wananchi waendelee na shughuli zao mbalimbali za ujenzi wa taifa ikiwemo kutekeleza haki yao ya kuabudu.” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amehimiza katika ujenzi wa taifa lenye umoja na mshikamano pamoja na kuwa na watu wanaoheshimiana na kuthaminiana.