Rais Samia apongezwa na kaya masikini

HomeKitaifa

Rais Samia apongezwa na kaya masikini

Wananchi mkoani Lindi jimbo la Mchinga wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na serikali ya awamu ya sita kwa ujumla jinsi anavyoonesha kwa vitendo kuzikomboa kaya masikini.

Wakizungumza wakati wa ziara ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, wananchi hao walioko katika kijiji cha Kilangala, wanaonufaika na fedha za kusaidia kaya masikini zinazosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), walisema kupitia fedha hizo wamejiinua kiuchumi kwa kubuni miradi mbalimbali ikiwemo kilimo cha minazi ambako wana shamba la ekari 15.

Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wenzake wa Kijiji hicho, ambao wanajihusisha na mradi wa kilimo Cha mazao mbalimbali ya biashara ikiwemo minazi, Dalini Makwaya, alisema wanatoa shukrani kwa Rais Samia kwa uamuzi wake wa kutoa fedha hizo na kuwafikia moja kwa moja wahusika na hivyo kubadilisha maisha yao.

“Tunamshukuru Serikali ya Rais Samia kwa kwa mpango huu kwa kuwa umetusaidia sisi kaya masikini, kupitia fedha hizo tumekata bima za afya, tunanunua sare za wanafunzi wetu na kubwa zaidi tunanunua chakula, kwa hili tunasema Asante Rais wetu,” amesema Makwaya.

Afisa wa mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) halmashauri ya Manispaa ya Lindi Bi. Dativa Kisima alimueleza Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi kuwa pamoja na kuwawezesha wananchi miradi hiyo ya kujipatia kipato kwa muda mrefu bado wamewapa ajira za muda kwa kuwalipa shilingi elfu tatu kwa siku kwa kila mmoja.

Akizungumza na wananchi hao, Shaka amesema kwa ushuhuda huo kuna kila sababu ya kuendelea kumshukuru Rais Samia ambaye amedhamiria kwa vitendo kuondoa umasikini kwa Watanzania kupitia TASAF kwa kushirikiana na wabia wa maendeleo huku akionesha matumaini makubwa kwa Mkoa wa Lindi akisema zinakwenda kuuinua zaidi kiuchumi.

“Rais Samia anayo dhamira ya dhati kabisa kuhakikisha kwamba anatumia kila fursa anayoipata pamoja na kushirikiana na wabia wa maendeleo anawatoa Watanzania katika dimbwi hili la umasikini.

“Mkuu wa Mkoa wa Lindi kupitia maelezo yake amesema kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kwa makusudi kuwekeza nguvu katika Mkoa huu wa Lindi ili kuleta mabadiliko, kwanza ya huduma za kijamii, lakini pili kuleta mabadiliko katika huduma hizi za kiuchumi na hilo linaonekana kwa macho kupitia miradi ya maendeleo tuliyoikagua leo,” alisema.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Tarek, amesema Mkoa huo ni wa kimkakati ambapo mazao yanayolimwa ni ya kibiashara akitolea mfano zao la minazi na korosho.

“Mwananchi akiwa na minazi anauhakika wa kila baada ya miezi mitatu kupata fedha. Lakini pia tuna zao la korosho ambalo ni zao linauzwa kibiashara duniani na ushahidi ukifika msimu wafanyabiashara kote duniani wanakuja mkoani Lindi kwa ajili ya kupata korosho namba moja inayopatikana mikoa ya Kusini. 

Kwa hiyo tulichokifanya tunaendelea kuwahamasisha wananchi wetu hawa wanaopata fedha za TASAF waingie kwenye kilimo hiki kwa sababu ukishaotesha minazi na ikaota vizuri unauhakika kabisa kwamba miaka yako yote ya maisha unauhakika wa kuvuna nazi au madafu na ukajipatia fedha.”

error: Content is protected !!