Rais Samia Suluhu Hassan amelitaka Jeshi la Polisi kuongeza kasi ya matumizi ya teknolojia katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuongeza ufanisi utakaochochea upatikanaji wa haki na weledi.
Matumizi ya teknolojia kwa taasisi za haki jinai ni miongoni mwa mambo yaliyowekewa msisitizo na tume ya haki jinai iliyofanya uchunguzi na kuainisha mapungufu yanayokwamisha utendaji kazi wa taasisi hizo muhimu nchini.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika ufunguzi wa kikao kazi cha maafisa waandamizi wa polisi, leo Septemba 4, 2023 amesema kuwa matumizi ya teknolojia yatakwenda kubadilisha na kuongeza ufanisi wa jeshi la polisi.
“Hii mifumo 13 ambayo tayari imeshasimikwa, tayari imeshaleta mageuzi na ufanisi ndani ya jeshi la polisi… nilikuwa na zungumza na IGP kanipa mfano ule mfumo wa mafaili, akilituma kwa kamishna lisipofanyiwa kazi mfumo unaonesha,” amesema Rais Samia jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Rais Samia mfumo huo utasaidia kuongeza uwajibikaji kwa kuwa mhusika atasalia kwenye kazi aliyopangiwa mpaka atakapoimaliza.
Aidha, ili kukamilisha zoezi la ufungaji wa mifumo ya teknolojia kwa haraka Rais Samia amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Camillius Wambura kutosita kumuomba fedha kama ameishiwa.
“IGP kama umeishiwa fedha ya kufunga mifumo mingine njoo tuzungumze ili nitafute fedha ya kukamilisha jambo hilo… umesema hapa mmeshasomana na Takukuru, mmeshasomana na DPP bado mahakama njoo tuzungumze…,” amesisitiza Rais Samia.
Kwa upande wake IGP Wambura amesema kuwa mifumo ya Tehama ambayo imeshafungwa ukiwemo wa ‘e- police’ umeshaonesha matokeo chanya ikiwemo kuongeza ufanisi, kupungua kwa gharama za uendeshaji wa ofisi, kupungua kwa upotevu wa majalada na kuwezesha ofisi kufanya kazi saa 24.
Hata hivyo Rais Samia amesisitiza jeshi hilo kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na maadili kwa kuwa bado amekuwa akipokea malalamiko yanayotokana na watendaji wasio waadilifu kwenye taasisi hiyo ambao wamekuwa wakijihusisha na rushwa pamoja na kubambikia watu kesi za uongo.