Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kwa waumini wa Kanisa Katoliki ndani na nje ya nchi kufuatia kifo cha Papa Francis aliyefariki dunia Jumatatu akiwa na umri wa miaka 88.
“Nimesikitishwa na taarifa ya kifo cha Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francisko. Ameishi kama mwalimu na kiongozi aliyehimiza amani, ustawi na maendeleo ya watu,” amesema Rais Samia kupitia ukurasa wake wa X.
Ameongeza kuwa kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Tanzania, anatoa pole na kumuombea Papa apumzike mahali pema.
Papa Francis aliongoza Kanisa Katoliki tangu mwaka 2013 na atakumbukwa kwa kuhimiza haki za binadamu, usawa na mshikamano wa kimataifa.