Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuungana na kukemea vitendo vya mauaji vinavyotokea nchini ili kukomesha matukio hayo badala ya kutoa shutuma na matusi kwa Serikali huku wakiacha jukumu la kudhibiti uhalifu kwa vyombo vya dola pekee.
Hivi karibuni kumeripotiwa matukio ya utekaji na mauaji ambapo baadhi ya wananchi wamenyooshea vidole vyombo vya dola kushiriki katika matukio hayo ikiwemo mauaji ya aliyekuwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyeuawa baada ya kutekwa kwenye basi la Tashrif akiwa safarini kuelekea mkoani Tanga.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Polisi Tanzania ameungana na Watanzania pamoja na jumuiya za kimataifa kulaani tukio hilo akiongeza kuwa uhai wa Mtanzania yoyote unathamani sawa bila kujali itikadi, kabila, rangi au umajumui wake hivyo linapotokea tukio lolote umma unatakiwa kuungana kukemea na si kwa baadhi ya watu pekee.
“Kifo cha ndugu yetu Kibao kimeibua wimbi kubwa, kulaani, kusikitika, kulaumu, kuita Serikali ya wauaji, hii sio sawa, kifo ni kifo, tunachotakiwa kufanya Watanzania wote tukemeane, tusimame imara kukemea mambo haya, damu ya Mtanzania ituume, tusiwe tunamwaga damu bila sababu,” amesema Rais Samia.
Rais Samia ameelezea masikitiko yake juu ya mauaji ya watu wenye ualbino, wazee, watoto, na wanafamilia akitaja matukio hayo kama ishara ya baadhi ya wanajamii kupoteza utu na kuongezeka kwa uhalifu mkubwa, ambapo hata watu mashuhuri na viongozi wa dini wamehusishwa hali inayowakatisha tamaa wananchi.
Kwa mujibu wa Rais, ili kukomesha mwenendo wa kujirudia kwa matukio ya mauaji, wananchi wanapaswa kutoa taarifa za matukio hayo ikiwemo ya kikatili pindi yanapotokea kwa kuwa matendo hayo hufanyika miongoni mwa wanajamii wenyewe, akisisitiza pia umuhimu wa polisi kuwa karibu zaidi na jamii ili kufuatilia matukio hayo.
“Lakini yanapotokea haya yanatokea kwenye maeneo yetu huko tunakaa kimya mpaka polisi iibuke iseme wengine hawasemi…inasikitisha kuona mambo haya ya mauaji yanatokea katika maeneo tunayoishi, inawezekana wananchi tunayaona lakini hatutoi taarifa na hapa ndio kunakuja ule umuhimu wa polisi kuweko kule kwa jamii katika kata husika ili kuweza kuyafuatilia kwa karibu zaidi,” amesema Rais Samia.