Vibanda umiza kusajiliwa na serikali

HomeKitaifa

Vibanda umiza kusajiliwa na serikali

Bodi ya Filamu Tanzania imeanza uhakiki wa vibanda umiza vilivyopo mtaani lengo ni kuvisajili na kuweka utaratibu wa undeshaji.

Pia wameunda Kamati maalum ya kuhamasisha Watanzania kurejesha utamaduni wa kuangalia filamu katika kumbi za sinema.

Katibu Mtendaji wa Bodi hiyo, Dk Kiagho Kilonzo ameyasema hayo leo Jumanne Oktoba 4, 2022 wakati akielezea utekelezaji wa shughuli za bodi na mwelekeo wa utekelezaji wa mwaka 2022/2023.

Amesema hivi sasa Tanzania kuna kumbi tisa ambazo ziko katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Tanga na Dodoma na kwamba Serikali haiwezi kuhamasisha uwekezaji katika eneo hilo bila kuongeza idadi ya watu wanaokwenda kwenye kumbi hizo.

Amesema mapato ya wasanii yatatokana na uwepo wa kumbi hizo ambapo kwa programu ya sasa na asilimia 45 ya mapato yanayotokana na kumbi hizo yamekuwa yakienda kwa wasanii.

 “Tumeishaanza kuvitambua. Na tayari timu yangu ipo kazini inapita kwa kushirikiana na maofisa utamaduni kujua kila mtaa kuna vibanda umiza vingapi na kuvisajili na baada ya hapo tutavipa utaratibu jinsi gani vinajiendesha,”alisema.

Aidha, Dk Kilonzo amesema kwa kupitia Kamati ya Kutetea Haki za Wasanii wamefanikiwa kurejesha Sh300 milioni kwa wasanii akiwemo marehemu King Majuto ambazo walidhulumiwa kutokana na mikataba mibovu.

Amesema pia bodi inataribu kamati maalumu ya kutetea haki za wasanii ambapo malalamiko 22 yamesuluhishwa huku nane yapo katika hatua mbalimbali za kushughulikiwa.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema katika sekta ya filamu kumekuwa na mafanikio makubwa kwani nchi imeweza kutangazwa.

 

SOURCE : MWANANCHI

error: Content is protected !!