Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea na jitihada za kuimarisha sekta ya ushirika na kilimo nchini kwa kuzindua benki ya kwanza ya ushirika, inayomilikiwa kwa asilimia 51 na vyama vya ushirika. Akizungumza katika uzinduzi wa benki hiyo, Rais Samia amesema kuwa ni hatua kubwa katika kurejesha hadhi ya ushirika nchini.
Benki hiyo yenye mtaji wa shilingi bilioni 58, itakuwa na jukumu muhimu katika kutoa huduma za kifedha kwa wanaushirika, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020-2025. Rais Samia alieleza kuwa hatua hii ni muhimu kwa kuongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha tija kwenye kilimo, hasa katika maeneo ya vijijini.

Rais Samia Suluhu Hassan akizindua mashine ya huduma za kifedha (Automated Teller Machine – ATM) kwa ajili ya Benki ya Ushirika Tanzania iliyopo Jijini Dodoma tarehe 28 Aprili, 2025.
Aidha, alieleza kuridhishwa kwake na jinsi wanaushirika wanavyohimili changamoto na kuongeza uzalishaji kutokana na huduma wanazozipata kutoka serikalini, ikiwemo ruzuku na msaada mwingine. Aliongeza kuwa benki hii itachochea maendeleo ya kilimo na kukuza usalama wa chakula.
Rais Samia pia alieleza matumaini kwamba benki hii itavutia taasisi zingine za fedha kuwekeza zaidi katika sekta ya ushirika na kilimo, ili kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa. Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kwamba sekta ya kilimo inakuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa.