Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Soko Kuu la Kariakoo, lililokuwa likifanyiwa ukarabati tangu mwaka 2022 kufuatia ajali ya moto mkubwa ulioteketeza mali zote zilizokuwa ndani ya jengo hilo.
Uzinduzi huo umefanyika leo, tarehe 8 Februari 2026, katika viwanja vya soko hilo jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na wafanyabiashara, wakazi wa jiji pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa.
Baada ya janga hilo, Serikali ilitenga shilingi bilioni 28 kwa ajili ya ukarabati wa soko hilo. Sehemu ya fedha hizo ilitumika kujenga soko msaidizi la ghorofa sita.
Ukarabati wa Soko Kuu umehusisha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya kudhibiti majanga ya moto, uwekaji wa huduma rafiki kwa watu wenye mahitaji maalum, pamoja na ufungaji wa lifti kwa ajili ya abiria na mizigo—hatua iliyolibadilisha Soko la Kariakoo kuwa kitovu cha biashara cha kisasa zaidi.




