Rais Samia Suluhu Hassan amesema Mkoa wa Kigoma utakuwa kituo cha utalii wa tiba na ametoa shiingi bilioni tano za kuanza ujenzi wa hospitali ya kanda.
Alisema hayo jana baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitalu ya Rufaa ya Maweni ambayo baadhi ya majengo ya huduma yamekamilika.
Rais Samia alisema serikali imeamua kuufanya Mkoa wa Kigoma kitovu cha biashara kwa ukanda huo hivyo inaendelea kuujenga sambamba na kuboresha miundombinu ya barabara, maji, afya, elimu na nyingine ili kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana.
“Sisi maono yetu tuwe na utalii wa afya, watu watoke nchi jirani waje kupata huduma za tiba hapa. Tanzania iwe kituo cha ubingwa wa mambo ya afya kwa nchi tunazopakana nazo, ndio maana nimetoa tena hizo sh bilioni tano kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya ya kanda hapa Kigoma,” alisema Rais Samia.
Pia, alisema Kigoma ni mkoa wa pembezoni mwa nchi na sasa wameufanya mkoa wa kimkakati wa biashara ndio maana serikali inahakikisha unapata umeme wa gridi wa uhakika ili ufungue fursa za uwekezaji.