Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amechaguliwa rasmi kuwa Balozi wa Huduma za Afya ya Mama na Mtoto barani Afrika, uteuzi uliotolewa na Kamati Kuu ya Africa CDC wakati wa kikao cha tano cha wakuu wa nchi cha utendaji cha Afrika CDC kilichofanyika leo Februari 09, 2026 kwa njia ya mtandao.
Katika kikao hicho, Dkt. Samia amewakilishwa na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ambaye alishiriki mjadala huo kwa niaba ya Tanzania akimbatana na wataalamu kutoka Wizara ya Afya pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, katika Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam.
Agenda kuu ya kikao hicho, kilichokuwa na agenda saba, ilikuwa ni kupokea na kuthibitisha taarifa ya Kamati Tendaji pamoja na mpango kazi wa Africa CDC kwa mwaka 2026
Uteuzi huo ni heshima kubwa kwa Tanzania na ni ishara ya kutambua mchango na uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha sekta ya afya, hususan kwenye kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto, ndani na nje ya nchi
Uteuzi wa Rais Samia kama Balozi wa Afya ya Mama na Mtoto unaendelea kuiweka Tanzania katika nafasi ya kipekee ya uongozi wa masuala ya afya barani Afrika, huku ukionyesha imani ya Afrika katika dira na jitihada zake za kulinda uhai wa mama na mtoto.


