Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema kwamba Tanzania itaendelea kukopa ili kukamilisha miradi na kuharakisha maendeleo.
Akihutubia leo hii mara baada ya kushudia utiani saini wa mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa (kipande cha Makutopora hadi Tabora) Rais Samia amesema kwamba kutokana na uwekezaji ambao tayari umefanyika kwenye mradi wa ‘SGR’, ni lazima Tanzania ikope.
“Uwekezaji mpaka sasa hivi ni Trilioni 14.7, tusipoendelea na ujenzi wa reli hii tukakamilisha, fedha hizi tulizozilaza pale chini zitakuwa hazina maana. Kwa hiyo kwa njia yoyote kwa vyovyote, tutakopa tutaangalia njia rahisi, njia zitakazotufaa za kukopa. Kwa sababu fedha hizi hatutazitoa kwenye tozo, wala hatutazitoa kwenye kodi tunazokusanya ndani. Ni lazima tutakopa. Kwa hiyo tutakopa ili kukamilisha mradi huu” amesema.
Aidha, Rais Samia Suluhu amesema kuna jitihada zinazofanyika ili kuvunja moyo suala ukopaji na pia wapo watu waliokuwa wanatamani kuona utekelezaji wa miradi unakwama ili wapate la kusema. Amesema Kuna jitihada za kutuvunja moyo kwenye mikopo. Hakuna nchi isiyokopa, hata hizo zilizoendelea wana mikopo mikubwa kuliko ya kwetu. Tutakopa tumalize miradi ya maendeleo ili tuendelee. Kwa sababu ukikopa unajenga sasa kwa haraka kuharakisha maendeleo. Ukisubiri ukusanye za kwako utamaliza lini kujenga? Mradi wa Matrilioni unasubiri ukusanye za kwako, utaumaliza lini?. Lakini kopa, tengeneza, kusanya nenda kalipe”
Vilevile Rais Samia maesisitiza kwamba miradi yote ya maendeleo inaendelea kutekelezwa na Serikali yake itaendelea kutafuta fedha ili kuikamilisha kwa wakati.