Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kutambua na kupongeza juhudi za maafisa ugani na maafisa ushirika katika kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini. Akizungumza katika mkutano na maafisa hao, Rais Samia aliwataja kama “mashujaa wasioimbwa” ambao mchango wao umekuwa na athari kubwa katika kufanikisha utoshelevu wa chakula nchini.
“Leo hapa wapo mashujaa wasioimbwa ambao pia wamekua mchango mkubwa kwenye mafanikio hayo nao si wengine ni maafisa ugani. Hawa ni mashujaa wasiosemwa na mtu lakini uhakika wa chakula tunaojivunia nao, asilimia 128 ya utoshelevu wa chakula unatokana na hawa watu,” alisema Rais Samia.
Rais alisisitiza kuwa serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya kilimo, na kwamba uwekezaji huo umeleta matokeo chanya, ikiwa ni pamoja na ongezeko la tija kwenye uzalishaji na mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa. Aliongeza kuwa utumishi wa maafisa ugani umetoa maana zaidi kwa uwekezaji huo mkubwa.
“Matokeo ya ongezeko la tija kwenye uzalishaji na kuongezeka kwa mchango wa sekta ya kilimo kwenye pato la taifa unachangiwa na maafisa ugani pia. Hivyo maafisa ugani nanyi mnastahiki pongezi kubwa sana,” alisema.
Rais Samia pia alizungumzia umuhimu wa kujenga uchumi jumuishi unaolenga maendeleo ya vijijini na kupunguza umaskini. Alieleza kuwa ongezeko la bajeti katika sekta ya kilimo lililenga kuongeza tija kwa matumizi ya mbolea, usambazaji wa mbegu bora, na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji maji.
“Muelekeo wa serikali yetu ni kujenga uchumi jumuishi, unaochochea maendeleo vijijini na kuongeza kasi ya kupunguza umaskini kwa wananchi mmoja mmoja lakini na jamii kwa ujumla,” aliongeza.
Kwa upande wa maafisa ushirika, Rais Samia aliwataka kuwa watetezi wa haki za wanachama wao badala ya kuwa wakandamizaji. Alisisitiza kuwa ushirika unatakiwa kusimamia maslahi ya mwanachama na kuhakikisha kuwa haki zao zinalindwa.
“Ushirika unatakiwa uwe mtetezi na msimamizi wa mwanaushirika, sio wewe uwe mbinyaji na mkandamizi wa haki ya mwanaushirika,” alisema Rais Samia.