Rais Samia: Membe alipenda maendeleo ya wananchi

HomeKitaifa

Rais Samia: Membe alipenda maendeleo ya wananchi

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kifo cha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Benard Membe, kimeacha pengo kubwa kwa familia, Watanzania na mataifa ya jirani aliyoyafanyia kazi ya kulinda utu pamoja na heshima ya mtu.

Rais Samia aliyekuwa akitoa salamu za rambirambi katika ibada maalumu ya kuuaga mwili wa Membe leo Mei 14, 2023 amewaambia Watanzania kuwa kifo cha Membe kimewasikitisha watu wengi ndani na nje ya taifa la Tanzania kwani alikuwa mtu mashuhuri na mwana diplomasia mahiri.

“Ndugu Membe alikuwa mtu muungwana sana, mchapakazi na aliyependa maendeleo ya nchi na wananchi wake, si tu katika taifa lake bali hata mataifa mengine…

Hivyo kifo chake kimeacha pengo kubwa sio tu katika familia, bali kwa taifa la Tanzania na mataifa ya jirani aliyoyafanyia kazi ya kulinda utu na heshima ya mtu,” amesema Rais Samia kwa huzuni.

Samia ameongeza kuwa kwake yeye Membe alikuwa ni kaka wa karibu aliyependa kufundisha na kutoa maarifa yake kwa wengine kwani wamefanya kazi pamoja katika Baraza la Mawaziri pamoja na Halmashauri ya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Pamoja na hayo, Rais Samia amesema anaungana na Watanzania wote kutoa salamu za Rambirambi kwa wafiwa na wote walioguswa na msiba huo kwani umewagusa watu wengi ndani na nje ya Tanzania kutokana na umahiri wa Membe katika uga wa diplomasia.

“Msiba huu si wenu peke yenu ni wetu sote, ingawa athari na machungu ya msiba huu kitakuwa upande wenu…, kwa hakika nguzo kuu imeondoka ninamuomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na awape subra wafiwa wote katika kipindi hiki cha majonzi mnachopitia,” amesema Rais Samia.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Stergomena Tax amesema Membe alifanya kazi kubwa ya kukuza diplomasia kati ya Tanzania na mataifa mengine pamoja na jumuiya za kikanda na kimataifa.

“Mchango wake katika kukuza uhusiano wa kimataifa na ujirani mwema kati ya Tanzania na mataifa mbalimbali nje ya bara la Afrika utaendelea kubaki kama historia njema ya taifa letu, wizara hii imenufaika sana na utumishi uliotukuka wa Membe na tutaendelea kumkumbuka na kumuenzi,”

Ibada ya kuuaga mwili wa Bernard Membe aliyefariki baada ya kuugua ghafla Mei 12, 2023 imefanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam ambapo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Tanzania, na wawakilishi wa jumuiya za kimataifa.

Kwa mujibu wa ratiba rasmi iliyotolewa na familia ya Membe, ibada ya misa takatifu itafanyika kesho Mei 15, 2023 katika kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam kisha utasafirishwa kwenda Mkoani Lindi, kwa ajili ya maziko ambapo atazikwa Mei 16, 2023 kijijini kwao Rondo katika jimbo la Mtama.

error: Content is protected !!