Rais Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imedhamiria kwa dhati kuwainua Wanawake kijamii, kiuchumi, kisiasa pamoja na kupambana na ukatili dhidi yao.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Miaka 50 na Kongamano la Wachungaji na Maaskofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania katika Chuo Kikuu cha St. John’s Jijini, Dodoma amesema Serikali inafanya hivyo sio kwa sababu kuwa yeye ni Rais mwanamke, bali kwa kuwa mwanamke ana haki sawa kama mwanaume isipokuwa kinachowatofautisha ni makuzi na imani zao.
Ameongeza kuwa wanawake hapa nchini kuwa wapo zaidi ya asilimia 50 hivyo kama wakiachwa nyuma maendeleo hayawezi kupatikana kwa urahisi.
Pia, ameeleza kuwa hapendi kuona mwanamke akiwekwa kama mtu wa daraja la chini na kubainisha kuwa dhamira yake kwa sasa ni kuwanyanyua wanawake na ameliomba kanisa hilo kumuunga mkono katika jitihada hizo.
Vilevile, Mhe. Rais Samia amelipongeza na kulishukuru Kanisa hilo la Anglikana Tanzania na kwamba mafundisho yanayotolewa na kanisa hilo kwa waumini wao pamoja na yale yanayotolewa na dini na madhehebu mengine ndio yanayosaidia nchi kuwa na amani, umoja na mshikamano.
Kanisa hilo ambalo lipo nchini kwa takribani miaka 176 lina mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za jamii ambapo lina vituo vya kutolea huduma za afya 40, vyuo vya afya 7 na taasisi za elimu 63, kikiwemo Chuo Kikuu cha St. John’s Jijini Dodoma.