Rais Samia Suluhu aonesha mfano kwa kutangaza kupunguza matumizi ya mafuta katika ofisi zake

HomeKitaifa

Rais Samia Suluhu aonesha mfano kwa kutangaza kupunguza matumizi ya mafuta katika ofisi zake

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa mfano wa moja kwa moja katika kupunguza matumizi ya mafuta kwa kuanzisha utaratibu mpya katika ofisi yake hatua ambayo ni sehemu ya jitihada za taifa kukabiliana na ongezeko la bei ya mafuta duniani.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha viongozi wateule katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Rais Samia amesema,

“Ndani ya serikali tuna matumizi makubwa sana ya mafuta, niwaombe sana tuanze kupunguza matumizi hayo. Nami naanza na ofisini kwangu; ninapotembea, maofisa wakubwa wote na magari yao wananifuata. Kuanzia sasa, maofisa wote hao nitawaingiza katika basi moja, kupunguza matumizi ya mafuta.”

Rais Samia amewataka watumishi wa umma na taasisi binafsi kuiga mfano huo katika maeneo yao kwa kupunguza safari zisizo za lazima na matumizi yasiyo na tija, hatua inayolenga kuokoa rasilimali na gharama za serikali.

Ameongeza kuwa ongezeko la bei ya mafuta duniani limeleta changamoto kwa uchumi wa mataifa mengi, ikiwa ni pamoja na Tanzania.

“Leo tumeamka na neno la faraja kwamba angalau pale Hormuz, meli zinapita, hivyo inatupa matumaini. Kwa kuruhusu meli za awali za Ufaransa na Japan kupita, tumeona bei ya mafuta kidogo imeshuka,” alisema Rais Samia.

Aidha, Rais amewahimiza wananchi na wafanyabiashara kuwa na utulivu na kuendeleza maisha yao ya kila siku bila kuathiriwa na mabadiliko ya soko la dunia, huku akisisitiza kuwa hatua za kupunguza matumizi ya mafuta ni jukumu la kila mtumishi na raia.

error: Content is protected !!