Rais Samia: Wananchi toeni maoni Dira ya Maendeleo 2050

HomeKitaifa

Rais Samia: Wananchi toeni maoni Dira ya Maendeleo 2050

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kushiriki katika mchakato wa maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya 2050 ili kupata dira jumuishi itakayokidhi mahitaji ya taifa katika kipindi cha miaka 25 ijayo.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika kilele cha tamasha la Kizimkazi, leo Agosti 31, amebainisha kuwa dira iliyopo hivi sasa inakaribia mwisho hivyo wananchi waanze kujiandaa kwa ajili ya dira mpya.

“Nipende kuchukua fursa hii kuwataka wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni kwaajili ya Dira ya Maendeleo ya taifa letu ya mwaka 2050, kama mnavyoelewa dira yetu ya maendeleo inaishia mwaka 2025,” amesema Rais Samia.

Dira ya Maendeleo ya Tanzania inayotamatika mwaka 2025, inaongozwa na malengo makuu matatu ambayo ni kuboresha hali ya maisha kwa wananchi wote, uongozi bora na utawala wa sheria, na kujenga uchumi imara na thabiti ambao unaweza kuhimili kikamilifu ushindani wa kimataifa.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El-Maamry utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 umewezesha Tanzania kuingia katika uchumi wa kati wa chini kwa kuongeza kasi ya ukuaji kwa asilimia 6 na kupungua kwa kiwango cha umaskini kwa zaidi ya asilimia 9 kutoka mwaka 2000 hadi 2018.

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango alipokuwa akizindua mchakato wa dira mpya ya maendeleo alibainisha kuwa maandalizi ya Dira mpya yazingatie matumizi ya fursa ambazo hazijatumiwa ipasavyo hadi sasa.

Mpango aliongeza kuwa dira hiyo ifungamanishwe na fursa zinazochipukia ikiwepo kilimo, mifugo na uvuvi, mazao ya misitu, uongezaji thamani ya mazao pamoja na uvunaji wa rasilimali za kimkakati na kujenga viwanda.

Sambamba na kuwataka wananchi kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa maandalizi ya dira mpya ya maendeleo, Rais Samia amewataka wadau mbalimbali kushiriki kupunguza ama kuziondoa changamoto za kimaendeleo.

error: Content is protected !!