Royal Tour yajibu, watalii zaidi ya 1,000 waja na meli

HomeKitaifa

Royal Tour yajibu, watalii zaidi ya 1,000 waja na meli

Ikiwa imepita miaka miwili tangu janga la Uviko-19 litikise dunia na shughuli za utalii kuanza kurejea, jana Tanzania ilipokea meli kubwa ya watalii zaidi ya 1,000 kutoka Marekani.

Meli hiyo inayofahamika kama Zaandam ina watalii 1,060 na wato huduma zaidi ya 500.

Meli hiyo inayomilikiwa na Kampuni ya Hollanda America Line, imetia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam kwa siku mbili kabla ya kuelekea Zanzibar ambako pia itakaa siku mbili.

Ujio wa meli hiyo unatajwa kama njia itakayosaidia kuchangamsha uchumi kwa kuliingizia taifa fedha za kigeni, hasa katika maeneo ambayo watalii hao watatembelea na kupata huduma.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Amos Nnko alisema hayo ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa ya kutangaza vivutio vya utalii kimataifa na ni fursa kwa sekta ya utalii.

“Serikali imefanya kazi kubwa ya kutangaza vivutio na hili limeonekana namna ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan alishiriki kwenye Royal Tour, kwa hiyo wageni hawa ni fursa kuwba kwa nchi kiuchumi.

“Niwasihi Watanzania wanaotoa huduma za utalii na wafanyabiashara kuchangamkia ziara hii na kutoa huduma bora ili kuwashawishi kurejea tena nchini au kuwavutia wengine waje,” alisema.

Watalii hao watatembelea Hifadhi ya Selous, mji wa kihistoria Bagamoyo na kuzunguka jiji la Dar es Salaam.

error: Content is protected !!