Royal Tour yaleta mafuriko ya watalii nchini

HomeKitaifa

Royal Tour yaleta mafuriko ya watalii nchini

Idadi ya watalii wanaokuja nchini baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kushiriki na kuongoza ziara za uzinduzi wa filamu ya Royal Tour nchini Marekani imezidi kuongezeka.

Aidha, viwanja vya ndege, hoteli na mbuga za wanyama zimeshuhudia ongezeko hilo la watalii ambao hawajawahi kutokea nchini.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Uendeshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KADCO), Christine Mwakatobe alisema watalii zaidi ya 1,700 kutoka Ulaya na Asia hushuka kila siku kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) na kwenda moja kwa moja katika hifadhi za taifa.

Alisema moja ya sababu za mafuriko hayo ya watalii wanaotua KIA ni filamu ya Royal Tour iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu na kuoneshwa sehemu mbalimbali duniani juu ya vivutio vya utalii vilivyoko nchini.

Mwakatobe alisema kwa zaidi ya miaka miwili hali ilikuwa ngumu juu ya kuja kwa watalii na hiyo ilitokana na kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19 ulioenea sehemu mbalimbali duniani kabla ya kupatikana chanjo.

Naye Katibu wa Chama cha Watoa Huduma za Utalii (TATO) Mkoa wa Arusha, Cyril Ako alisema asilimia kubwa ya wageni wanaokuja nchini ni wale waliohamasishwa na filamu ya Royal Tour na kutokana na idadi hiyo hata kampuni za utalii zimekumbwa na uhaba wa magari ya kuwapeleka watalii mbugani.

error: Content is protected !!