Sababu 5 zinazoweza kupelekea jengo la ghorofa kuporomoka

HomeMakala

Sababu 5 zinazoweza kupelekea jengo la ghorofa kuporomoka

Baada ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa lilikokuwa likijengwa katika eneo la Goba kwa Awadhi jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo na majeruhi, watu wengi wanaweza kujiuliza sababu zinazoweza kupelekea kuanguka kwa jengo, hususan jengo la ghorofa.

Click Habari inakujulisha baadhi ya sababu zinazoweza kupelekea kuporomoka kwa majengo;

1. Msingi dhaifu

Msingi wa jengo ni kati ya sehemu zenye gharama kubwa zaidi katika ujenzi, lakini pia ni hatua muhimu sana katika uimara wa jengo.

Antony Ede ambaye ni mhandisi wa majengo kutoka Chuo Kikuu cha Covenant nchini Nigeria, aliwahi kuhojiwa na BBC na kueleza kwamba msingi imara lazima uzingatie aina ya udongo pamoja na kuwa vipimo sahihi juu ya uzito wa jengo linalotarajiwa kujengwa. Alieleza kwamba baadhi ya wajenzi huamua kubana matumizi kwenye ujenzi wa msingi, jambo ambalo ni hatari sana, kwani nchini Nigeria kuna majengo mengi yaliyowahi kuanguka kwa sababu hiyo.

Msingi unaweza kugharimu nusu ya fedha zinazotumika katika ujenzi, lakini ni vyema kutumia gharama zote hizo kwa uimara wa jengo.

2. Udhaifu wa vifaa vya ujenzi

Taasisi moja inyaoundwa na wahandisi kutoka nchi mbalimbali za Afrika, iitwayo ‘African Organization for Standardization, iliketu jijini Nairobi mwaka 2916 na kujadili sababu za za kuporoka kwa majengo barani Afrika. Katika mkutano wao, mkandarasi Hermogene Nsengimana alisema majengo mengi yameporomoka kwa sababu ya kutumika kwa vifaa dhaifu, akitolea mfano wa mjengo yaliyoporomoka mwaka 2016 nchini Uganda.

Wakandarasi wanaweza kuamua kutumia vifaa vyenye ubora wa chini kwa lengo la kupunguza gharama, jambo ambalo limegharimu hata maisha ya watu katika baadhi ya nchi hususan za Afrika.

3. Makosa ya wafanyakazi

Vibarua wanaotumika katika ujenzi, wanaweza kupewa majukumu mbalimbali lakini washindwe kuyatekeleza kama walivyoelekezwa na wataalam.

Hili linaweza pia kuchangiwa na wajenzi kuamua kutumia vibarua ambao hawana stadi za kutosha ili wawalipe ujira mdogo. Sababu hiyo ilielezwa vizuri mwaka 2004 jengo moja refu lilipoporomoka nchini Uganda. Utafiti uliofanywa na wahandisi Henry Mwanaki na Stephen Ekolu ulionesha wkamba vibarua walishindwa kuchanganya zege katika ubora uliotakiwa.

Jengo linaweza kuondoa maisha ya wengi, hivyo ni bora kuwalipa watu wenye ujuzi ili kupata jengo imara.

4. Uzito mkubwa kuliko ilivyotarajiwa

Mwaka 2014, jengo la aliyekuwa mhubiri mashuhuri wa nchini Nigeria, marehemu TB Joshua lilianaguka na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 100. Taarifa kuhusu chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo zilieleza kwamba jengo hilo liliongezewa ghorofa (floors) nyingi kuliko ilivyotarajiwa.

Jengo lingine liliporomoka nchini Nigeria mwaka 2016 mwezi Machi na kusababisha vifo vya watu 34, sababu ikielezwa kwamba lilielemewa na mzigo.

Watu huweza kuamua kubadili matumizi ya jengo, na hivyo kuongeza uzito kwenye msingi. Hilo linaweza kufanya jengo liporomoke.

5. Kushindwa kupima uimra wa jengo.

Wataalam wa majengo hutumia mbinu mbalimbali kupima uimara wa jengo kila baada ya hatua fulani ya ujenzi. Hilo lisipofanyika katika hatua zinazopaswa, uwezekano wa makosa kugundulika kwa kuchelewa ni mkubwa, na inawea kupelekea jengo kuporomoka.

Kwa ujumla zipo sababu nyingi zinazoweza kupelekea jengo kuporomoka lakini ‘ubahili’ (kubana matumizi kupitiliza) una nafasi kubwa sana kwenye kufanya majengo yaporomoke. Watu wanakwepa gharama za ujenzi zinazotakiwa, matokeo yake wanaingia hasara kubwa zaidi majengo yanapoporomoka.

error: Content is protected !!