Sababu 6 za Oman kuwekeza Tanzania

HomeKimataifa

Sababu 6 za Oman kuwekeza Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan jana ametoa sababu sita za wafanyabiashara wa Oman kuwekeza nchini Tanzania, kwa kuwa inatoa fursa za pekee za uwekezaji.

Akihutubia katika Kongamano la Biashara baina ya Oman na Tanzania mjini Muscat, Rais Samia amesema Serikali yake inajipanga kwa utekelezaji wa kuwezesha uwekezaji kwa wepesi.

Rais Samia ametaja uhusiano wa kihistoria wa kindugu, amani, utulivu, utawala bora na mazingira mazuri, sera thabiti za uchumi na fedha, upatikanaji wa soko katika bara la Afrika, uwepo wa wafanyakazi wenye ujuzi wa kati pamoja na uwepo wa njia rahisi na za haraka ndizo zilizochangia uwekezaji wa Oman nchini Tanzania.

Rais Samia amebainisha kuwa biashara na uwekezaji wa nchi hizo mbili umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, lakini jitihada zaidi zinahitajika katika kuweka usawa wa kibiashara.

Rais Samia amesema kuongezeka kwa uwekezaji kumeinufaisha Tanzania, ambapo hadi Aprili 2022 ilisajili miradi 62 ya uwekezaji kutoka Oman yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 308.35 na kutoa ajira 2,489.

Raia kutoka Oman wamewekeza Tanzania katika sekta za kilimo, ardhi na majengo, ukandarasi, madini, rasilimali watu, utalii, viwanda, huduma, uchukuzi, mawasiliano na Miundombinu.

Rais Samia yuko nchini Oman kwa mwaliko wa Sultan wa Oman, Haitham bin Tariq Al-Said.

 

error: Content is protected !!