Sababu za watumishi kukosa nidhamu

HomeKimataifa

Sababu za watumishi kukosa nidhamu

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kukosekana kwa mafunzo ya kada mbalimbali za utumishi wa umma ni miongoni mwa sababu zinazochangia kutetereka kwa maadili ya watumishi ikiwemo ukosefu wa nidhamu.

Rais samia ameyasema hayo leo Mei 21, 2022 Ikulu, Chamwino Jijini Dodoma alipokuwa akiwaapisha viongozi wateule walioteuliwa Mei 11 mwaka huu wakiwemo manaibu katibu wakuu wa wizara pamoja na makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma.

Ili kurejesha nidhamu kwa watumishi wa umma, Rais Samia amemtaka mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Hamisa Hamis Kalombola kurejesha utaratibu wa kutoa mafunzo ya utumishi wa umma ili kuwakumbusha wajibu wao na kuongeza  nidhamu na uwajibikaji katika ofisi za umma.  

“Tunataka utumishi ambao mtu atakuwa na itikadi moyoni mimi ni mtumishi wa umma, ethics (maadili) yangu ni hizi, mstari wangu ni huu hapa, kwa hiyo naomba mkasimamie sana..” amesema Rais Samia.

Sambamba na hayo, Rais Samia amesisitiza suala la haki sawa kwa Watanzania wote ambapo ameitaka Tume ya Utumishi wa Umma kutoegemea upande wowote na kuajiri wale wote wenye sifa na vigezo vinavyostahili.

Viongozi wateule walioapishwa leo ni manaibu katibu wakuu ambao ni Dk Charles Msonde aliyeapishwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Tamisemi na Dk Maduhu Kazi kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Jaji mstaafu  Hamisa Hamis Kalombola ameapishwa kuwa  Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma na Makamishna  ambao ni Balozi John Michael Haule, Immaculata Peter Ngwalle, Ali Mohamed Mbarak, Susan Paul Mlawi, Balozi Adadi Mohamed Rajab, pamoja na Nassor Nassa Mnambila.

 

 

error: Content is protected !!