Mgombea wa Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, akihutubia wananchi wa Kibaigwa, Wilaya ya Kongwa, amekumbusha utekelezaji wa ahadi alizotoa katika awamu yake ya kwanza, akibainisha kuwa matokeo yake yanaonekana wazi kupitia miradi mikubwa ya maendeleo.
Katika sekta ya elimu, mbali na ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari, serikali imekamilisha ujenzi wa Chuo cha VETA Kongwa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.3, ambacho kimewawezesha vijana kupata ujuzi wa fani mbalimbali kwa ajili ya kujiajiri na kuajiriwa. Idadi ya shule za sekondari imeongezeka na kufikia 45, huku sera ya elimu bila ada ikiendelea kutekelezwa kwa mafanikio makubwa.
Sekta ya afya imeimarika kupitia ujenzi wa vituo vipya 14 vya afya, na kufanya jumla ya vituo kufikia 73. Aidha, jengo jipya la huduma za dharura katika hospitali ya wilaya lenye thamani ya shilingi bilioni 4.5 limekamilika na kufungwa vifaa tiba vya kisasa, ikiwemo mashine mpya ya X-ray.
Kwa upande wa nishati, vijiji vyote vya Kongwa sasa vina umeme, huku jitihada zikiendelea kuhakikisha huduma hiyo inafika kwenye vitongoji, taasisi na kaya zote. Sub-station mpya iliyokamilika sasa inahudumia Gairo, Mpwapwa na Kongwa, hatua iliyosaidia kuondoa changamoto ya upungufu wa umeme.
Sekta ya maji nayo imeboreshwa kupitia uchimbaji wa visima 61, huku dhamira ya awamu ijayo ikiwa ni kuhakikisha tatizo la maji safi na salama linaondolewa kabisa kwa wananchi wote.
Katika miundombinu ya barabara, kilomita za lami zimeongezeka kutoka 3.7 mwaka 2021 hadi 11.7 mwaka 2025. Aidha, barabara ya Bonde la Mtanana yenye urefu wa kilomita 6 itaboreshwa ili kudhibiti mafuriko. Pia, serikali imepanga kujenga vituo vya afya kumi na zahanati 21, sambamba na kukamilisha hospitali ya wilaya.