Serikali imetoa Sh milioni 180 zilizotumika katika ujenzi na kukamilisha ukarabati mkubwa wa vyumba tisa vya madarasa na uwekaji umeme katika shule kongwe ya msingi ya Kilosa Town iliyoanzishwa na wakoloni mwaka 1917, wilayani Kilosa, Mkoa wa Morogoro.
Kaimu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Lusia Msese amesema hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa madarasa mapya tisa ya kisasa yaliyojengwa kutokana na mpango wa serikali kuboresha shule kongwe nchini.
Msese amesema shule hiyo ambayo mwaka huu 2023 imefikisha miaka 106 tangu ianzishwe, ilikuwa na vyumba nane, lakini sasa ina jumla ya vyumba 17 vya madarasa.
Amesema kabla ya serikali kutenga fedha na kufanyika ukarabati huo mkubwa, majengo yake yalikuwa ni uchakavu, sehemu ya paa kuvujisha maji na kuta zikiwa na nyufa nyingi.
Msese amesema kuwa, shule hiyo ambayo kwa sasa ina wanafunzi 793 iliyokuwa na mkondo mmoja kwa kila darasa kutokana na uchache wa vyumba vya madarasa , madawati na uchakavu wa majengo yake ilisababisha hali ya utoro kwa wanafunzi.