Serikali kuongeza pensheni kwa wastaafu

HomeKitaifa

Serikali kuongeza pensheni kwa wastaafu

Serikali ya Tanzania imesema itaongeza malipo ya mkupuo ya kikokotoo cha pensheni ya wastaafu kutoka asilimia 33 iliopo sasa hadi asilimia 40 lengo likiwa ni kuimarisha maslahi ya watumishi hao.

Mabadiliko haya yanakuja ikiwa ni siku 42 tu tangu Makamu wa Rais Dk Philip Mpango aahidi maboresho katika suala hilo huku akisistiza kuwa maboresho hayo yatatokana na tathmini ya kina ya kisayansi ya watakwimu bima. Dk Mpango aliyasema hayo Mei 1, 2024 alipokuwa akihutubia katika siku ya wafanyakazi duniani iliyofanyika kitaifa jijini Arusha.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa akiwasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25 bungeni Dodoma leo Juni 13, 2024 amesema kuwa maamuzi hayo yamefikiwa kutokana na kuwepo kwa malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa watumishi hao.

“Serikali yetu sikivu inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan, imesikia kilio hicho na imekifanyia kazi kwa maslahi mapana ya wastaafu wetu na wanaotarajiwa kustaafu… ameelekeza kuongezwa malipo ya mkupuo kutoka asilimia 33 iliopo sasa hadi asilimia 40,” amesema Dk Mwigulu.

Waziri huyo amesema ongezeko hilo ni kwa watumishi waliokuwa wakilipwa asilimia 50 hapo awali ambao walishushwa hadi asilimia 33, ikiwa ni theluthi tu ya penshen yao.

Kwa upande wa watumishi waliokuwa wakipokea malipo ya mkupuo ya asilimia 25 hapo awali na kupandishwa kwenda asilimia 33, Dk Nchemba amesema sasa itakuwa asilimia 35 kuanzia mwaka huu wa fedha unaoanza Julai mosi.

Huenda mabadiliko haya yakafuta machozi ya watumishi pamoja na wabunge wao waliokuwa wakipaza sauti bungeni wakitaka Serikali kuongeza kikokotoo hicho na ikiwezekana wastaafu wapewe zaidi ya asilimia 50 ya mafao yao ili kujiendeleza kiuchumi.

error: Content is protected !!