Bia, michezo ya kubahatisha kugharamia bima ya afya kwa wote

HomeKitaifa

Bia, michezo ya kubahatisha kugharamia bima ya afya kwa wote

Serikali imependekeza ongezeko la ushuru kwa viwango tofauti kwenye michezo ya kubahatisha, bidhaa za urembo, vinywaji laini, bia na pombe kali ili kuongeza mapato yatakayotumika kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo wakiwemo watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa akiwasilisha Bajeti ya Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 Juni 13, 2024 Bungeni jijini Dodoma amependekeza kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye thamani ya dau la kamari (value of the stake on betting) kwenye michezo ya kubahatisha na bahati nasibu ya Taifa.

“Hatua hii inatarajia kupeleka kiasi cha Sh 29.52 bilioni katika Mfuko huo (Mfuko wa Bima ya Afya),” amesema Dk Mwigulu.

Waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibu amependekeza kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye ada ya matangazo ya biashara za michezo ya kubahatisha na bahati nasibu ya Taifa yanayotangazwa kupitia vituo vya televisheni, redio, na tasnia ya uchapishaji.

Amesema lengo la hatua hiyo ni kuongeza wigo wa kodi ambapo inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh9.15 bilioni.

Bia kuchangia bima ya afya

Dk Mwigulu pia amependekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 ili kuelekeza asilimia 2 ya mapato ya ushuru wa bidhaa yanayokusanywa kutoka kwenye bidhaa za urembo, vinywaji laini (carbonated drinks) na vileo (bia na pombe kali) kwenye bima ya afya kwa wote.

“Hatua hii inatarajia kupeleka kiasi cha Sh18.8 bilioni katika mfuko huo,” amesema Mwigulu.

Fedha zitakazopatikana ushuru utakaotozwa katika maeneo hayo mawili zitasaidia kuongeza fedha zitakazotumika kwa ajili ya kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo na makundi maalum hususan wanawake wajawazito na watoto wa umri chini ya miaka mitano.

Dk Nchemba amesema Bunge lilipitisha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote Na. 13 ya mwaka 2023 ambapo Serikali inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wake.

Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) ambao unatarajia kutumia Sh446.3 bilioni kwa mwaka wa fedha ujao, hivi karibuni uliibua mjadala mkali kwenye jamii na mtandaoni baada ya uamuzi wake kufuta kifurushi cha bima kwa watoto walio chini ya miaka 21 (Toto Afya).

NHFI ilidai kuwa kifurushi hicho kilikuwa kinaiongezea mzigo na hivyo kushauri wazazi kutumia vifurushi vingine kuwasajili watoto wao katika mfuko huo wa bima hususan kupitia shuleni.

error: Content is protected !!