Serikali imesema imesaini mikataba minne yenye thamani ya Sh bilioni 681.53 kwa ajili ya kuboresha huduma ya usafiri katika mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) maarufu ‘mwendokasi’.
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba alisema hayo bungemi Dodoma jana alipokuwa akiwasilisha bajeti kuu ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha 2025/2026.
Dk. Mwingulu alisema mikataba hiyo ni ushirikiano baina ya sekta ya umma na sekta binafsi, yenye lengo la kuongeza ufanisi kiutendaji katika uendeshaji na utoaji huduma kwenye mfumo wa mabasi hayo.
“Napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kwamba mikataba minne ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) imesainiwa katika mwaka 2024/2025 kwa ajili ya kutoa huduma ya usafiri wa mabasi katika mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT),” alisema.
Aidha, Dk Mwigulu alianisha maeneo ambayo mradi wa mabasi hato umejumuisha ikiwemo ule wa awamu ya kwanza wa Kimara hadi Kivukoni na matawi yake ya Gerezani hadi Morocco ambayo ilishaanza tayari. Pia, awamu ya pili ya mradi huo ambayo ni Mbagala hadi Morocco kupitia Chang’ombe na Mbagala hadi Gerezani ambayo bado ipo kwenye hatua ya ujenzi wa miundombinu.
Ili kuboresha utoaji wa huduma za jamii, Dk. Mwigulu alisema serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.