Serikali yaongeza posho za safari

HomeKitaifa

Serikali yaongeza posho za safari

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuupiga mwingi kwa kutoa kibali cha kurekebisha posho ya kujikimu ya safari za ndani ya nchi kwa Watumishi wa Umma na kiwango cha malipo ya kazi maalum (Extra Duty) kwa Watumishi wa Umma nchini ambapo utekelezaji wake unaanza rasmi tarehe 01 Julai, 2022.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro jijini Dodoma wakati wa Kikao Kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma chenye lengo la kutathmini utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Dkt. Ndumbaro amesema kutokana na kibali hicho cha Mhe. Rais, posho ya kujikimu ya safari za ndani ya nchi kwa Watumishi wa Umma kwa kiwango cha juu imepanda kutoka shilingi 120,000/= hadi 250,000/= na kiwango cha chini kutoka shilingi 80,000 hadi 100,000/=.

Ameongeza kuwa, kiwango cha malipo ya kazi maalum (Extra Duty) kwa Watumishi wa Umma kimeongezeka kwa ngazi zote, ambapo kwa ngazi ya chini kimepanda kutoka shilingi 15,000/= hadi 30,000/=, kwa ngazi ya kati kimeongezeka kutoka shilingi 20,000/= hadi 40,000/= na kwa ngazi ya juu kimeongezeka kutoka shilingi 30,000 hadi 60,000/=.

Dkt. Ndumbaro amesisitiza kuwa, viwango hivyo vipya vitalipwa na Serikali kupitia bajeti iliyoidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023, hivyo taasisi zisiombe nyongeza ya bajeti ili kuwalipa viwango hivyo watumishi wake.

Kufuatia ongezeko hilo, Dkt. Ndumbaro ametoa wito kwa Watumishi wa Umma wote nchini kufanya kazi kwa bidii, maarifa, weledi na nidhamu ya hali ya juu ili kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Mhe. Rais za kuboresha masilahi wa Watumishi wa Umma.

“Watumishi wa Umma tuwajibike kwa hiari bila kushurutishwa, tuwe wabunifu zaidi ili kutoa mchango katika maendeleo ya taifa na ustawi wa nchi kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuhakikisha tunatatua kero zinazowakabili wananchi,” Dkt. Ndumbaro amesisitiza.

error: Content is protected !!