Jumla ya Sh bilioni 298 zimetumika na serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26 kuongeza nguvu manunuzi ya dawa na vifaa tiba ili kufidia fedha zilizokuwa zikitumika kupambana na magonjwa ya Kifua Kikuu, UKIMWI na Malaria nchini.
Hayo yamesemwa jana Julai 21 na Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Grace Magembe, wakati wa kikao kazi cha kupitia bajeti ya Mfuko wa Dunia ‘Global Fund’ ambapo serikali imefikia hatua hiyo ili kwenda sambamba na mahitaji ya Watanzania kufuatia baadhi ya nchi kupunguza ufadhili wake.
“Mtakumbuka hivi karibuni kuna fedha ambazo baadhi ya nchi wahisani zimepunguza ufadhili wake katika kuhudumia Magonjwa ya kifua kikuu, UKIMWI na Malaria ili kupambana na magonjwa hayo nchini, hata hivyo serikali kwa uharaka imetoa Dola za kimarekani Milioni 54 sawa na Sh bilioni 140 za kitanzania kwa mwaka wa fedha 2024/25,” amesema Dk. Magembe
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26 serikali iliongeza fedha hizo ili kukidhi mahitaji zaidi ya mwananchi wa chini ambao wamekuwa wakisumbuliwa na magonjwa hayo.
“Mwaka huu wa fedha wa 2025/26 serikali pia imeongeza Dola millioni 60 sawa na Sh bilioni 159 za kitanzani kwa ajili ya magonjwa kufidia hayo mapungufu ya fedha ambayo yametoka kwa nchi wahisani, lengo kuu la haya yote ni kuhakikisha tunaboresha ubora wa huduma kwa wananchi na wahitaji kutoka maeneo mbalimbali,” amesema Dk. Magembe
Kikao kimekutanisha wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wakiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu, OR-Tamisemi, Wizara ya Fedha na Wizara ya Afya, Ubalozi wa Marekani pamoja na washirika kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni, Tanzania National Coordinating Mechanism (TNCM) na Local Fund Agent (LFA), huku lengo kuu likiwa ni kujadili namna ya matumizi ya rasilimali zinazopatikana kuendana na mahitaji ya jamii.