Rais Kagame na ziara ya kikazi Tanzania

HomeKimataifa

Rais Kagame na ziara ya kikazi Tanzania

Mheshimiwa Paul Kagame, Rais wa Jamhuri ya Rwanda atafanya Ziara ya Kikazi nchini kuanzia tarehe 27 hadi 28 April, 2023.

Mheshimiwa Rais Paul Kagame na Ujumbe wake unatarajia kuwasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) tarehe 27 Aprili 2023 na kupokelewa na Mheshimiwa Dkt. Stergomena Tax (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Akiwa nchini, Mheshimiwa Rais Kagame atakutana na kufanya mazungumzo na Mwenyeji wake, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, IKULU Jijini Dar es Salaam, tarehe 27 Aprili 2023. Aidha, Viongozi hao Wakuu wataongea na Waandishi wa Habari kuelezea yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo yao.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Rwanda zimekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliodumu kwa muda mrefu ambapo nchi hizi mbili zimekuwa zikishirikiana kwenye sekta mbalimbali za kimkakati ikiwemo biashara na uwekezaji, nishati, uchukuzi, elimu na utamaduni.

Kufanyika kwa ziara hii ni ishara nzuri ya kuendelea kuimarika kwa uhusiano wa kidugu baina ya mataifa haya kwa maslahi mapana ya pande mbili.

error: Content is protected !!