Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amekerwa na danadana zinazoendelea katika kupata utatuzi wa mgogoro wa ardhi kati ya wakazi wa eneo la kiwanja cha ndege mkoani Mtwara na mamlaka ya viwanja vya ndege.
Akizungumza alipotembelea eneo hilo kufuatilia maelekezo aliyoyatoa alipotembelea eneo hilo , Shaka amesema danadana hizo hazina tija kwa wananchi na kutoa maelekezo kwa wizara nne kukutana haraka ili kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo.
“Ndugu zangu mimi nilisema nije na kuja kwangu ni kuweka msisitizo kwamba Chama kinafuatilia kwa karibu sana mgogoro huu, baina ya wananchi na mamlaka ya viwanja vya ndege na mamlaka zingine ambazo zimeingia katika kadhia hii.
“Kama kuna upande una haki, kama kuna upande hauna haki lakini unahitaji huruma basi mamlaka zinazokaa zikae zipime zitafakari uzito wa kuusaidia huo upande na athari endapo watausaidia huo upande ni zipi na mwisho waje na majibu ili wananchi hawa waishib kwa amani, ili wananchi hawa waishi kwa utulivu.
“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ipo pamoja na ninyi, na ipo pamoja na ninyi katika kuhakikisha mgogoro huu unafikia mwisho,” amesema.
Amesema wizara nne zinahusika katika utatuzi wa mgogoro huo, hivyo ameziagiza kukutana haraka iwezekanavyo ili kuutafutia ufumbuzi na kwamba kama zimeshindwa kutatua basi waeleze ili suala hilo lipelekwe katika ngazi za juu zaidi.
“Ukifuatilizia hapa kuna karibu wizara tatu zinaingia kwa nne. Wizara ya Uchukuzi ambao ndio wana mamlaka ya viwanja vya ndege, wizara ya Nishati ambao wao wana dhamana ya gesi, wizara ya tamisemi ambao wao wana watu na wizara ya ardhi ambao wamepewa mamlaka ya kisheria kusimamia mambo ya ardhi…sasa taasisi moja inapokuwa mlalamikaji kwamba wenzake hawapo tayari kutoa ushirikiano ni jambo linalosikitisha sana ndugu zangu huko serikaliini.
“Maelekezo ya Chama ni kwamba, taasisi hizo nne nilizozitaja zikutane haraka sana kujadili kadhia hii na waje na majibu ya kuwapa wananchi hawa,” ameagiza.
Shaka ametoa agizo hilo baada ya Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Mkoa wa Mtwara, Samuel Miruma kusema kusuasua kwa utatuzi wa mgogoro huo kunachangiwa na baadhi ya taasisi zinazohusika kuchelwa kutoa ushirikiano.