Shilingi bilioni 5 zatengwa kuimarisha kampuni 50 za TEHAMA

HomeKitaifa

Shilingi bilioni 5 zatengwa kuimarisha kampuni 50 za TEHAMA

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetekeleza kwa vitendo ahadi ya kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa biashara ndogo, za kati na Kampuni Changa (Startups) ndani ya siku 100 za uongozi wake, kwa kutenga Shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kuziimarisha Kampuni changa za TEHAMA.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dodoma jana Februari 4, 2026 Waziri Kairuki amesema fedha hizo zitatolewa kupitia benki za biashara kwa Kampuni Changa 50 zitakazokidhi vigezo vilivyowekwa, huku mpango huo ukitekelezwa katika wizara saba.

Amesema kampuni zitakazonufaika ni zile zinazojihusisha na sekta ya Fedha (FinTech), Afya, Kilimo (Agri-Tech), Elimu (Edu-Tech), Utalii, Bima, Akili Unde (AI), Logistics na Lishe.

Ameeleza kuwa wizara ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha makubaliano na benki za biashara ili kuhakikisha mikopo hiyo inapatikana kwa riba nafuu, jambo litakalosaidia kampuni changa kuwekeza zaidi katika rasilimali watu, miundombinu na kuimarisha usalama wa mifumo yao ya kidijitali.

Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, kukua kwa kampuni changa kunatarajiwa kufungua fursa mpya za ajira kwa vijana, ambapo kila kampuni inaweza kuajiri watu kati ya saba hadi 10, hivyo kuongeza kipato cha kaya, kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza mapato ya Serikali.

Amewahimiza vijana wabunifu kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwasilisha maombi yao mara tu tangazo litakapotolewa kuanzia Februari 11, 2026 kupitia mitandao ya kijamii ya Wizara na jumuiya za Kampuni Changa, baada ya kukamilika kwa vigezo rasmi vitakavyohakikisha uwazi na usawa kwa waombaji.

Aidha, amesema ndani ya siku 100 hizo Wizara imeanza maandalizi ya kuanzisha Mfuko wa Kitaifa wa Uwezeshaji wa Kampuni Changa za TEHAMA pamoja na kukamilisha Rasimu ya Sera ya Kampuni Changa ya Mwaka 2026, hatua zitakazoweka mazingira rafiki ya biashara, kukuza bunifu, kuongeza ajira na kuvutia uwekezaji wa TEHAMA ndani na nje ya nchi.

error: Content is protected !!