Shule ya kimataifa ya Wakimbizi kujengwa Tanzania

HomeKitaifa

Shule ya kimataifa ya Wakimbizi kujengwa Tanzania

 

Balozi wa Shirika la Elimu, Utamaduni na Sayansi la Umoja wa Nchi za Kiarabu, Amiri Fehri anakusudia kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuomba ridhaa ya kujenga shule ya kimataifa kwa ajili ya wakimbizi watoto nchini Tanzania.

Balozi huyo kijana (17) na maarufu duniani, raia wa Tunisia alibainisha hayo alipokutana na kufanya mazungumzo hivi karibuni na Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Irene Kasyanju.

“Naomba kupatiwa nafasi ya kukutana na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan ili kumuomba nasaha zake (moral support) katika kampeni yangu ya kusambaza “salamu ya Amani na Uvumilivu duniani”, lakini zaidi kuomba ridhaa ya Mheshimiwa Rais ili niweze kujenga shule yenye hadhi ya kimataifa kwa ajili ya wakimbizi-watoto nchini Tanzania”, Balozi Fehri alisema.

Akielezea kuhusu matarajio yake hayo, alisema shule hiyo itakuwa inatoa vyeti vya kimataifa ili kuwasaidia watoto hao ama kupata kazi nchini Tanzania au wakirejea katika nchi zao.

Aidha Fehri ameomba apatiwe nafasi ya kukutana na wanafunzi wa shule na vyuo mbalimbali nchini Tanzania ili kuwaelimisha kuhusu unyanyasaji unaofanyika mashuleni (bullying) na madhara yake pamoja na njia za kukabiliana na kadhia hiyo.

Kwa upande wake, Balozi Kasyanju alimpongeza Balozi Fehri kwa jitihada zake thabiti na kumshukuru kwa mapenzi yake juu ya Tanzania, lakini zaidi kwa dhamira yake ya kujenga shule ya wakimbizi nchini Tanzania.

Balozi Fehri anashirikiana na Rais wa Tume ya Ulaya, kupitia Mfuko wa Amir Fehri (Amir Fehri Foundation) kufungua shule ya kwanza ya Kimataifa huko Mosul, Iraq. Shule hiyo itakuwa ishara halisi ya elimu kwani itajengwa ndani ya kambi za wakimbizi na itatoa nafasi mpya kwa watoto wote wakimbizi.

error: Content is protected !!