Ikiwa leo dunia inaadhimisha siku ya kimataifa ya Mama Sayari dunia hii leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kufanyika kwa kila liwezekanalo kumlinda mama huyo kwa kuwa yuko mmoja tu na hakuna mbadala.
Guterres kupitia ujumbe aliotoa leo Aprili 22, 2022 amesema Dunia anakabiliwa na majanga matatu ambayo yanahitaji udharura kuyatokomeza ambayo ni mabadiliko ya tabianchi, kutoweka kwa bayonuai na mazingira halisi na uchafuzi na taka.
“Majanga haya matatu yanatishia ustawi na uhai wa mamilioni ya watu duniani kote. Misingi ya ujenzi wa maisha yenye afya, furaha, maji safi, hewa safi na tabianchi tulivu imetawanyika, na kuweka malengo yetu endelevu mashakani,” amesema Guterres.
Ametaka siku ya leo itumike kutathmini ubinadamu na sayari dunia akisema ukweli ni kuwa wakazi wa dunia wamekuwa walinzi dhaifu wa nyumba yao iliyo tete.
Hata hivyo, kuna matumaini kwa kuwa miaka 50 iliyopita serikali duniani zilikutana katika mkutano wa kimataifa wa Stockholm ambao amesema ulikuwa ni mwanzo wa harakati za mazingira duniani.
“Tangu wakati huo, tumeona kinachowezekana tukishirikiana pamoja. Tumeweza kupunguza tundu la ozoni. Tumeongeza wigo wa ulinzi wa wanyamapori na mifumo anuwai. Tumatokomeza matumizi ya nishati chafuzi, na kuzuia mamilioni ya vizazi mfu.
“Na mwezi uliopita tu, tulizindua juhudi za kihistoria za kimataifa za kuzuia na kutokomeza uchafuzi utokanao na plastiki,” amesema.
Ametaka hatua zaidi kuhakikisha kuwa ongezeko la joto halizidi nyuzi joto 1.5 katika Selsiyasi hivyo “serikali lazima ziwe zimepunguza uchafuzi kwa asilimia 45 ifikapo mwaka 2030, na ziache kabisa uzalishaji wa hewa ya ukaa mwaka 2050.”
Wachafuzi wakuu wa hewa lazima wapunguze kwa kiwango kikubwa kwa kuachana na uraibu wa nishati kisukuku na kuongeza kasi ya kutumia nishati jadidifu.
Pamoja na hatua hizo, Katibu Mkuu ametaka uwekezaji wa haraka kwenye uhimili, mnepo hususan kwa nchi masikini zaidi na zilizo hatarini ambazo zimesababisha kidogo janga hili.
Mwezi Juni, dunia inakutana tena Sweden kwa ajili kutathmini hatua zilizofikiwa kuilinda dunia kwa miaka 50 tangu mkutano wa Stockholm ufanyike.
“Viongozi wetu wanakuja na hatua za kijasiri kutatua majanga matatu ya dharura ya sayari dunia. Kwa sababu tuna Mama Sayari dunia mmoja. Tufanye kila tuwezalo kumlinda,” amesisitiza Guterres.