TAMISEMI imetoa ufafanuzi kuhusu alichokiwasilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, Innocent Bashungwa katika wasilisho la Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 jana bungeni, kwenye Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2021/22.
“Sehemu ya Huduma za Ustawi wa Jamii iliandikwa kuwa ‘ununuzi wa pikipiki 68 zenye thamani ya shilingi milioni 789.9 kwa ajili ya Maafisa Ustawi wa Jamii kwenye ngazi ya Kata umefanyika na kusambazwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa’ hivyo kuonekana kuwa pikipiki moja ilinunuliwa kwa takribani shilingi milioni 11 gharama ambayo si sahihi”
“Usahihi ni kuwa pikipiki zilizonunuliwa zilikuwa 268 na pikipiki zilizopokelewa kwa awamu ya kwanza ni 68 ambazo zimesambazwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, tunaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza” Taarifa hiyo ilisema.