Tanzania mwenyeji mkutano mkubwa Afrika wa chakula na kilimo

HomeKitaifa

Tanzania mwenyeji mkutano mkubwa Afrika wa chakula na kilimo

Huenda Afrika likaanza kujitosheleza kwa chakula siku zijazo baada ya wadau wa maendeleo na wataalam wa sekta ya kilimo kukutana Tanzania ili kujadili namna ya kupata suluhu ya uhakika na usalama wa chakula barani humo.

Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa Afrika wa masuala ya chakula na kilimo (AGRF) utakaofanyika Septemba 5 hadi 8, 2023.

AGRF ni jukwaa kuu la kuendeleza ajenda ya kilimo na mifumo ya chakula ambapo msisitizo utawekwa kwa vijana na wanawake kama msingi wa mfumo endelevu wa chakula barani Afrika.

Mkutano huo wa kila mwaka utawakutanisha watu zaidi ya 3,000 wakiwemo viongozi, watunga sera, wanasayansi, wakuu wa serikali na taasisi za binafsi, wakulima, na vijana ili kujadili na kutafuta suluhu ya usalama wa chakula barani Afrika na maisha bora kwa wote.

Maandalizi yaanza

Kesho Machi 17, Rais Samia Suluhu Hassan atazindua maandalizi ya mkutano huo Ikulu jijini Dar es Salaam, hii ni kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Zuhura Yunus.

Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo kutokana na hatua kubwa za kimageuzi ambazo Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imezichukua tangu alipoingia madarakani miaka miwili iliyopita.

Hatua hizo ni pamoja na kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo mara nne kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Serikali ya Rais Samia pia imetambuliwa kwa mradi wake wa ubunifu wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), ambao unalenga kuwawezesha vijana, ambao ndiyo nguvu kazi kubwa nchini, kuingia katika sekta ya kilimo.

Serikali yake pia imewekeza katika miundombinu ya umwagiliaji, huduma za ugani, pembejeo na ruzuku ya mbolea na mbegu kwa viwango vya juu ili kuimarisha sekta ya kilimo kwa maendeleo ya nchi.

Serikali ya Tanzania pia imekuwa ikitekeleza mpango wa kilimo unaojulikana kama Ajenda 10/30 wenye lengo la kufanya kilimo kiwe cha biashara na kikue kwa wastani wa asilimia 10 kwa mwaka ifikapo 2030.

error: Content is protected !!