Tanzania na Falme za Kiarabu zasaini mkataba kuondoa utozaji kodi mara mbili

HomeKimataifa

Tanzania na Falme za Kiarabu zasaini mkataba kuondoa utozaji kodi mara mbili

Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zimesaini makubaliano ya kuondoa utozaji kodi mara mbili, wadau wametoa maoni tofauti kuhusu faida na hasara za mikataba ya aina hiyo.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisaini mkataba huo na wa kuzuia ukwepaji wa kodi ya mapato akiiwakilisha Tanzania pamoja na Waziri wa Fedha wa UAE, Mohamed Bin Had Al Hussain.

Makubaliano hayo yanalenga kuhamasisha uwekezaji utakaochochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha kipato cha wananchi wa pande hizo mbili.

Waziri Nchemba alisema kusainiwa kwa mkataba huo ni jitihada za kuondoa changamoto za biashara ili kukuza mahusiano ya kiuchumi, kuimarisha ushirikiano wa kodi na kuchochea mazingira wezeshi ya uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

“Ni matumaini yetu kwamba baada ya mkataba huu tutaona uwekezaji mkubwa ukikua kati ya nchi zetu hizi, hasa kutoka Uarabuni ambao wana mitaji mikubwa, lakini utozaji kodi mara mbili ulikuwa unawakwaza,” alisema Dk Nchemba.

Mkataba huo wa makubaliano ya kodi ni wa 10 kwa Tanzania. Mingine ni kati ya Tanzania na Afrika Kusini uliosainiwa mwaka 2005, Canada 1995, nchi za Scandinavia zinazojumuisha Denmark, Finland, Norway, Sweden zote mwaka 1976, India 1979, Italia 1973 na Zambia 1969. UAE yenyewe imeingia mkataba kama huo na nchi 139.

Kuhusu mkataba huo

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru alisema: “Baadhi ya watu wanaweza kutafsiri kuwa mikataba ya aina hii ni kusamehe kodi, la hasha, hii ni mikataba inayoweka kanuni ya kuzuia uhamishaji wa kodi kutoka nchi moja kwenda nyingine kwa kuzingatia uwekezaji unatoka katika eneo gani, inahusisha kulinda mitaji ya wawekezaji wa nchi husika,” alisema Mafuru.

Kwa mujibu wa mtandao wa Tranding Economics, biashara baina ya Tanzania na UAE ilikadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Marekani 871 milioni (wastani wa Sh2.001 trilioni).

Baadhi ya bidhaa zinazohusika zaidi ni vito, madini, mbogamboga, dawa za asili, samaki, kahawa, chai, viungo, matunda, manukato na vipodozi.

error: Content is protected !!