Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amekutana kwa pamoja na kufanya mazungumzo na mabalozi wa Ufaransa, Italia na Uswisi.
Waziri Mulamula amekutana na Balozi wa Ufaransa nchini Mhe. Nabil Hajlaoui, Balozi wa Italia nchini Mhe. Marco Lombardi pamoja na Balozi wa Uswisi hapa nchini Mhe. Didier Chasot katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na nchi zao katika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na utunzaji wa mazingira.
Waziri Mulamula amewahakikishia mabalozi hao kuwa Serikali ipo tayari wakati wote kushirikiana na nchi zao katika utunzaji wa mazingira pamoja na mabadiliko ya tabia nchi.
“Serikali ya awamu ya sita imetoa kipaumbele katika utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi,” amesema Balozi Mulamula.
Nae Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Hajlaoui kwa niaba ya mabalozi wengine, amesema wanafurahishwa na jitihada za Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na utunzaji wa mazingira.