Wagonjwa wa mawe kwenye figo nchini hususani waliopo maeneo ya karibu na mkoa wa Dar es Salaam wamehimizwa kujitokeza katika kliniki ya siku tatu ya upasuaji wa kuondoa mawe kwenye figo kwa wagonjwa wenye changamoto hiyo kwa kutumia njia ya kisasa ya mionzi ya ‘laser’.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Hospitali ya Taifa Muhimbili – Mloganzila kambi hiyo ya upasuaji imeanza jana Januari 21 na inatarajia kumalizika Januari 23, 2026.
“Kambi hii inafanywa na wataalamu wa ndani waliobobea katika upasuaji wa mfumo wa mkojo na hii ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha huduma za kibingwa na kibingwa bobezi nchini.”
Taarifa hiyo imeendelea kufafanua kuwa hatua hiyo inatokana na uhitaji wa huduma hiyo kwa wananchi wengi hivyo kliniki hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wananufaika na uwekezaji mkubwa uliyofanywa na serikali katika sekta ya afya .
“Huduma ya kuvunja mawe kwenye figo kwa kutumia mionzi ya laser ni matibabu ambayo humsaidia mgonjwa kupata maumivu kidogo ,kutokuwa na kovu wala kukatwa ambapo mgonjwa atakaa wodini kwa siku mchache takribani siku moja hadi mbili na inahusisha wagonjwa wenye mawe kwenye figo madogo hadi ya kati, wagonjwa ambao dawa hazikusaidia, wanaoogopa upasuaji mkubwa, wagonjwa wenye uzito mkubwa au matatizo ya damu na wanaopata mawe ya figo mara kwa mara” Inasomeka sehemu ya taarifa hiyo
Wataalamu wa hospitali hiyo wakiongozwa na Dkt. Isaka wamesema kuwa wananchi wanaweza kujikinga na kupata mawe kwenye figo kwa kunywa maji mengi angalau lita 3 kwa siku, kupunguza matumizi ya chumvi nyingi, kupunguza nyama nyekundu kupita kiasi, kula matunda na mbogamboga, kufanya mazoezi na kufanya uchunguzi wa mara kwa mara.


