Serikali imesema mikakati ya kukabiliana na athari za vita katika eneo la Ukraine pamoja na uwekezaji katika sekta za kilimo, nishati, maji, ujenzi, madini na usafirishaji ilichochea kukuza uchumi kwa asilimia 5.4 mwaka 2024 kutoka asilimia 5.1 mwaka 2023.
Kiwango hiki ni juu kidogo ya wastani wa asilimia 4.4 uliotazamiwa mwaka 2023 kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na asilimia 3.8 kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema katika Taarifa yake ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 aliyoitoa Bungeni mjini Dodoma leo Juni 13 kuwa Pato halisi la Taifa lilifikia Sh bilioni 148,399.76 mwaka 2023 kutoka Sh bilioni 141,247.19 mwaka 2022.
“Ukuaji huo ulichangiwa na: jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ikiwemo mikakati ya kukabiliana na athari za vita kati ya Ukraine na Urusi pamoja na uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya nishati, maji, afya, elimu na usafirishaji,” alisema.