Tanzania na Kenya zapanga kuondoa vikwazo 14 vya biashara

HomeKimataifa

Tanzania na Kenya zapanga kuondoa vikwazo 14 vya biashara

Huenda uchumi wa Tanzania na Kenya ukakua zaidi kwa siku za usoni mara baada ya viongozi wakuu wa mataifa hayo kuwaagiza mawaziri wa biashara na uwekezaji kushughulikia vikwazo 14 vya kibiashara vilivyopo.

Rais Samia Suluhu Hassan amewaambia waandishi wa habari ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 10, 2022 kuwa awali katika jitihada za kuondoa vikwazo vya kibiashara kati ya Tanzania na Kenya walifanikiwa kuondoa vikwazo 54 kati ya 68 visivyo vya kikodi.

“Bado kuna vikwazo 14 vimebaki  tumewataka mawaziri wetu wa sekta ya biashara na uwekezaji wakutane haraka kufanyia kazi vikwazo 14 ili tuwe na uhuru mpana wa kufanya biashara,” amesema Rais Samia.

Amesema ziara ya Ruto inatoa fursa ya kutathimini fursa ya ushirikiano katika ngazi zote huku akitaka mataifa hayo kugawana utajiri utakaofanyika kupitia biashara.

Rais wa Kenya William Ruto ambaye alikuwa akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili hapa nchini kufuatia mualiko wa Rais Samia amesema kuondolewa kwa baadhi ya vikwazo vya kibiashara kumezinufaisha nchi zote mbili.

“Katika kipindi cha mwaka mmoja thamani ya bidhaa zinazosafirishwa kutoka Kenya kwenda Tanzania imeongezeka kutoka shilingi za Kenya bilioni 31 hadi bilioni 45 ambazo ni sawa na Sh868.3 bilioni za Tanzania,” amesema Ruto.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Samoei Ruto, mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 10 Oktoba, 2022.

Ruto ameongeza kuwa thamani ya bidhaa kutoka Tanzania kwenda Kenya nayo imeongengezeka kutoka Sh24 bilioni hadi Sh50 bilioni za Kenya ambayo ni sawa na Sh964.8 za Tanzania.

Katika kuimarisha uchumi Ruto amesema ataharakisha mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Mombasa ili kuchochea shughuli za kiuchumi na kupunguza  gharama za nishati.

“Tunaweza kuongeza kasi ya ufanyaji wa biashara kati ya mataifa yetu mara mbili zaidi ya ilivyo sasa, tunatarajia hadi mwezi Disemba vikwazo vilivyosalia vitakuwa vimefanyiwa kazi,” amesema Ruto.

Aidha, kutokana na kukithiri kwa vitendo vya uhalifu kama uharamia, usafirishaji haramu wa watu na madawa ya kulevya  mataifa haya yamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya ulinzi na masuala mengine ya kikanda na kimataifa.

Ruto amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili nchini Tanzania akitokea  nchini Uganda ambako alihudhuria maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa  taifa hilo ambako aliiasa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuungana kwa kufungua mipaka kwa raia wake.

Ziara hiyo ni ya kwanza kwa Ruto nchini Tanzania tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Kenya Septemba 13 mwaka huu.

error: Content is protected !!