Serikali ya Uingereza kupitia Ubalozi wake Tanzania imetangaza kupunguzwa kwa vikwazo vilivyokuwa vimewekwa kwa wasafiri wote kutoka nchini Tanzania.Taarifa iliyotolewa imeeleza kuwa vikwazo hivyo vitaondolewa kuanzia Jumatatu ya 11 Oktoba 2021.
Taarifa hiyo ina maana kwamba kuanzia tarehe tajwa wasafiri kutoka Tanzania wataondolewa katika orodha ya nchi ambazo wasafiri wake hawaruhusiwi kuingia nchini Uingereza.
Hatua hii haina maana kwamba masharti yote ya kusafiri baina ya nchi hizo yameondolewa moja kwa moja bali imeelezwa kuwa hitaji la kukaa karantini litaondolewa kwa wale tu waliopata moja kati ya chanjo nne zinazotambulika na Serikali ya Uingereza.
Taarifa toka Ubalozi huo imeeleza kufurahishwa na hatua zinazochukuliwa katika utoaji chanjo nchini huku ikifafanua kuwa inachukua hatua za haraka kupitia mfumo wa utoaji wa vyeti vya chanjo ili kuweza kutambua vyeti vinavyotolewa hapa nchini.
Ubalozi wa Uingereza Tanzania unatarajia kutoa maelezo zaidi juu ya hatua hizo, lakini kwa sasa umesisitiza kutembea tovuti ya www.gov.uk/coronavirus kwa taarifa zaidi.