Kipande cha ujenzi wa reli ya kati Tabora- Kigoma kitagharimu dola za Marekani bilioni 2.7 sawa na shilingi trilioni 6.34.
Reli hiyo ambayo mkataba wake umesainiwa jana Desemba 20, 2022 SGR LOT 6 (Tabora – Kigoma) katika Ukumbi wa Kikwete – Ikulu jijini Dar es Salaam, itachukua miezi 48 kukamilika.
Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mkataba wa kipande hicho, Mkurugenzi wa Shirika la Reli nchini (TRC), Masanja Kadogosa, amesema serikali itakuwa imewekeza dola za Marekani bilioni 10.04, sawa na Sh trilioni 23.3 kwa maana ya awamu ya Dar-Mwanza na Tabora-Kigoma.
Amesema utiaji saini huo unafanya utimilifu wa reli ya kati, kutoka Dar- Mwanza na Dar-Kigoma, kwingine kote kutakapofuata ni reli za matawi.