Ushirikiano: Siri ya mafanikio Kenya na Tanzania

HomeKimataifa

Ushirikiano: Siri ya mafanikio Kenya na Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameeleza mambo aliyozungumza na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. William Ruto ambaye yupo nchini kwenye ziara za siku mbili.

Akizungumza na waandishi wa wahabari Ikulu jijini Dar es Salaam leo tarehe 10 Oktoba, 2022, Rais Samia Suluhu amesema mambo yafuatayo.

KUKUZA NA KUIMARISHA UHUSIANO

Rais Samia amesema wamekubaliana na Rais Ruto kuendeleza ushirikiano na kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizi mbili ili kuwezesha ufanywaji biashara na kudumisha umoja.

“Tanzania na Kenya ukiacha mipaka ya kiutawala lakini mambo mengi tupo wamoja, tuna mpaka mkubwa watu wetu wanashirikiana watu wetu ni ndugu biashara zinakwenda mambo yetu ni mamoja kwahiyo tumekubaliana kukuza na kuimarisha uhusiano na ushirikano.” amesema Rais Samia.

USHIRIKIANO KATIKA BIASHARA

Rais Samia amesema ushirikiano mzuri katika biashara baina ya Tanzania na Kenya umefanikisha kuondolewa kwa vikwazo 54 kati ya 68 huku 14 vilivyobaki vinafanyiwa kazi ili kuhakikisha biashara na uwekezaji unafanyika bila vikwazo.

“Wataalamu walitambua vikwazo 68, ambavyo vilifanyiwa kazi vikwazo 54 viliondoka visivo vya kikodi na bado kuna vikwazo 14 vimebaki. Na tumetaka mawaziri wetu wa sekta ya biashara na uwekezaji wakutane kwa haraka wafanyie kazi vikwazo 14 ili tuwe na uhuru mpana sasa wakufanya biashara .” amesema Rais Samia.

MASUALA YA KUSAFIRISHA WATU

Pia, Rais Samia amesema wamekubalina na Rais Ruto kuhakikisha wanafanyia kazi suala zima la usafirishaji watu ambalo linaleta sifa mbaya kwenye nchi hizo mbili.

“Tumekuwa tukipata sifa mbaya ya human trafficking (usafirishaji watu) wakati wanaosafirishwa sio Watanzania sisi tunakamata tu lakini wakifika kwetu rekodi za dunia zinaiona Tanzania au kenya kwahiyo inabidi tuangalie vizuri.” amesema Rais Samia.

USHIRIKIANO MASUALA YA KIKANDA

Aidha. Rais Samia pia amesema wamekubaliana kuendeleza ushirikiano wao kikanda na katika Umoja wa Afrika ili kuwa mfano bora kwa wanachama wengine.

“Tumekubaliana kuendeleza ushirikiano mzuri na madhubuti kwenye Umoja wa Afrika kule UN lakini hasa ndani ya Afrika Mashariki kwamba Kenya, Tanzania na Uganda ndio viongozi wakubwa wa Jumuiya hii kwahiyo hatuna budi kushirikiana ili wanaoungana nasi wakute kuna ushirikiano madhubuti uliojengwa nasi.” amesema Rais Samia.

error: Content is protected !!