Usithubutu kufanya mambo haya 5 ‘wikiendi’ hii.

HomeElimu

Usithubutu kufanya mambo haya 5 ‘wikiendi’ hii.

Tangu wiki inapoanza, akili za wanadamu wengi huwaza zaidi mwisho wa wiki ili waweze kupumzika na kupata wasaa mzuri wa kufurahi na ndugu, jamaa na marafiki. Ijumaa inapofika, wengi huhisi wameachiliwa kutoka katika vifungo vya kazi, na kuwa huru kwenda katika njia za furaha yao kwa siku mbili.

Katika uhuru wako wa wikiendi, kuna mambo ni vyema ukaachana nayo kabisa ili kuweza kukamilisha furaha yako.

Click Habari inakushauri kuachana na mambo haya matano unapofurahi ‘wikiendi’ yako.

1. Kushindwa kupanga

Usiwe mtu wa ‘kudandia treni kwa mbele’, wala usiwe ‘bendera fuata upepo’. Weka mipango yako kuhusu namna unavyotaka ‘wikiendi’ yako iende.

Utakuwa na furaha zaidi pale ambapo utakuwa unaenda mahali ulipopanga kwenda, na kutumia kiasi cha fedha ambacho ulipanga baadala ya kukurupuka.

2. Kushindwa kujifikiria wewe.

Ulikuwa na wiki nzima ya kuwaza zaidi kuhusu kazi, kwa nini usitumie siku mbili kujijali wewe mwenyewe?. Waswahili husema “raha jipe mwenyewe”.

Ni vyema ‘wikiendi’ ikawa wakati wa kujijali : nenda saluni kidogo, some vitabu kama unapenda kufanya hivyo, tembelea fukwe, kula chakula ukipendacho na mambo mengine yataisuuza nafsi yako.

3. Kulala sana

Kuna mtazamo kwamba ukitumia muda mwingi kulala, unaweza kufidia zile siku ambazo hujapata muda wa kutosha kulala. Yani kama katikati ya wiki ulikuwa unachelewa kulala na kuwahi kuamka, unaweza kujipa moyo kwamba “Jumamosi nitalipa usingizi wangu”.

Hakuna utafiti wowote unaounga mkono hoja ya ‘kulipa usingizi’. Mtandao wa ‘Scientific American’ unaeleza kwamba kulala sana Jumamosi, hakufanyi ‘ulipe’ usingizi uliopoteza Alhamisi.

Usipoteze muda mwingi sana kwenye usingizi, utapoteza nafasi ya kufanya au kuona mambo mengine ambayo yangekupa furaha ya kweli mwishoni mwa wiki.

4. Kufanya mambo kupita kiasi

Kama unakunywa pombe, furahia ‘mvinyo wako ndugu’. Muimbaji mmoja anasema “Sio hatia kutumia fedha zako”, na kama pombe ndiyo matumizi yenyewe uliyochagua, kunywa. Tena sio mbaya kama utashushia na wimbo wa mwanamuziki Marioo ‘Bia Tamu’.

Hata hivyo, fahamu kiasi chako, usinywe kupitiliza ukajiweka kwenye hatari ya kukutwa na mambo ambayo hutamani yatokee.

Pombe ni mfano mmoja tu, mambo mengine yote lazima yafanywe kwa kiasi.

5. Kufanya kazi siku nzima

Watu wengi wanatamani jioni ya Ijumaa inapofika waachane kabisa na kazi zote. Lakini kwa bahati mbaya kuna kazi nyingi ambazo unaweza kujikuta una majukumu ya kufanya hata Jumamosi na Jumapili.

Lakini pia kazi za ‘wikiendi’ zinaweza kuwa kazi zako binafsi ambazo hukuweza kuzifanya katikati ya wiki.

Ni muhimu kupanga ratiba yako na kufahamu kwamba unahitaji kupumzika, unahitaji saa kadhaa nje ya kazi.  Panga muda wako, ‘tafuta hela’ lakini Jumamosi na Jumapili ziwe na muda wa kupumzika

error: Content is protected !!