Bandari ya Tanga kwa mara ya kwanza imeandika historia baada ya kupokea Meli ya MV PARNIA yenye Makontena 463 kutoka Iran.
Akiongea mara baada ya kupokea meli hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Dkt. Balozi Batilda Burian, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika bandari hiyo na matunda yake kuonekana.
“ Nampongeza Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono makubwa ya kuwekeza katika Bandari ya Tanga na leo hii tumeandika historia katika bandari hii kwa kupokea meli yenye Makontena mengi jambo ambalo halikuwahi kutokea huko nyuma kabla ya maboresho” Aliongeza Balozi Burian.
Aidha Balozi Burian alisema kuwa ujio wa meli hiyo katika Bandari ya Tanga kutoka Iran, ni fursa kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga na Mikoa mingine kufungua fursa za kibiashara baina ya Tanzania na Iran kwa kupitishia mizigo yao katika Bandari ya Tanga.
Katika hatua nyingine Balozi Burian aliahidi kuendelea kujenga ushirikiano wa kibiashara na Iran kwa kutumia bandari ya Tanga ili kuhudumia nchi za Afrika Mashariki na nchi za Ukanda wa SADC.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Dadi Kolimba alisema kuwa ujio wa meli hiyo katika Bandari ya Tanga ni fahari kwa wananchi kwani uchumi wa Tanzania utazidi kukua na fursa za kibiashara zitazidi kufunguka zaidi.
Awali akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa, Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga Bw. Peter Millanzi alisema kuwa kwa muda mrefu Bandari ya Tanga ilikuwa inapokea meli ndogo ndogo “Feeder Vessels “ kutoka Bandari za nchi jirani sababu bandari ilikuwa haina uwezo wa kupokea meli kubwa za makontena. Hata hivyo kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika kwa sasa Bandari ya Tanga ina uwezo wa kupokea meli kubwa na sasa historia imeandikwa ya kupokea meli kubwa za makontena kutoka moja kwa moja nchini Iran.
Meli hiyo yenye urefu wa mita 174 na kina cha mita 10.3 imetia nanga katika Bandari ya Tanga ikiwa na makontena 463, ambapo makontena 261 yakiwa ni ya Tanzania na makontena 182 yakwenda katika nchi za za Rwanda, Zambia, Malawi na Uganda.



