Taliban tayari wamejihakikishia rasmi taifa la Afghanistan liko chini yao hivyo mipango na kila kitu ndani ya taifa hilo itatokana na matwakwa yao. Wakati wameketi Kabul wanatafakari namna ya kuunda Serikali yao, wanagundua kuna mwiba mkubwa bado kwenye nyayo ambao ni kizingiti kikubwa kwao kuunda serikali kwa amani.
Mwiba wenyewe ni kundi la Pashnjir ambalo lipo Kaskazini Mashariki mwa mji wa Kabul ambalo linaipinga vikali serikali ya Taliban.
Mkuu wa kundi la Taliban, Amari Khan Motaqi amewaamuru watu wa Pashnjir wasalimishe silaha zao, lakini hakuna dalili kuwa watafanya hivyo. Pashanjir ni mchanganyiko wa makabila mbalimbali ya Afghanistan pamoja na wanajeshi walioasi jeshi la serikali ya Afghanistani.
Jeshi la Pashnjir limeundwa na aliyekuwa Makamu wa Rais Mtaafu wa nchi hiyo, Amrulla Saleh, lakini kwa sasa linaongozwa na Ahmad Massoud.
Taliban na viongozi wa kundi hilo wamekuwa na mazungumzo ya mara kwa mara na wote wameonesha nia ya kutotaka vita licha ya kutokuwa na makubaliano rasmi ya kimkataba kuzuia vita.
Duru mbalimbali zinaeleza kuwa muda wowote vita inaaweza ikaanza tena, huku Pashnjir ikitarajia kupata msaada kutoka nchi za Ulaya na Taliban kutoka Pakistan, Urusi na Qatar.
Pashanjir ni moja ya majimbo madogo ndani ya Afghanistan lenye watu kati ya 150,000 na 200,000, lililopo milimani usawa wa futi 9,800 kutoka Mto Pashnjir.