Mvutano unaoendelea kati ya Iran na Israel unaonekana kwa macho ya kawaida unaweza kudhani ni tatizo la mashariki ya kati pekee, lakini kwa Tanzania, linaweza kuwa na athari kubwa kiuchumi, hasa kupitia bei ya mafuta duniani. Baada ya Taifa la Marekani kushambulia vinu vya nyuklia vya Taifa la Iran usiku wa kuamkia leo, Bunge la Iran limepitisha uamuzi wa kufungia Strait of Hormuz, mlango mwembamba wa bahari unaopitisha zaidi ya asilimia 20 ya mafuta yanayosafirishwa dunia nzima. Hatua hii, endapo itatekelezwa, inaweza kusababisha bei ya mafuta kupanda kwa kasi, hali itakayoumiza uchumi wa nchi zinazoagiza mafuta kutoka nje ikiwemo Tanzania.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2023, Tanzania huagiza mafuta kutoka kwa nchi kama Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), India, Saudi Arabia, Kuwait, na Oman. Mafuta haya husafirishwa kwa meli kupitia Bahari ya Hindi baada ya kupita kwenye Mlango wa Hormuz. Kwa hiyo, endapo njia hii itafungwa, usambazaji wa mafuta unaweza kucheleweshwa au kusimama kabisa, jambo ambalo linaweza kuathiri upatikanaji na bei ya mafuta nchini.
Kwa sasa, bei ya mafuta aina ya Brent imepanda kutoka dola 65 (172,631/-) hadi takriban dola 77 (204,501/- ) kwa pipa. Wachambuzi wa masoko ya mafuta wanasema iwapo mvutano huu utaendelea na kuathiri usafirishaji, bei zinaweza kupanda hadi kati ya dola 100 (265,586/-) hadi 120 (318,704/-) kwa pipa. Kwa Tanzania, hali hii inaweza kuongeza gharama ya uagizaji mafuta kwa mabilioni ya shilingi, na kuongeza shinikizo kwenye bajeti ya serikali.
Kupanda kwa bei ya mafuta huathiri moja kwa moja gharama za maisha. Nauli za usafiri huongezeka, bei za vyakula hupanda kwa sababu ya gharama za usafirishaji, na huduma mbalimbali kama afya na elimu huathirika pale ambapo bajeti ya serikali inalazimika kuelekezwa kwenye sekta ya nishati. Kwa wananchi wa kawaida, hili lina maana ya mfumuko wa bei na kushuka kwa uwezo wa kununua mahitaji ya msingi.
Zaidi ya hayo, endapo hali hii itaendelea kwa muda mrefu, inaweza kuathiri hata thamani ya shilingi ya Tanzania kutokana na kuhitaji dola nyingi zaidi za kuagiza mafuta. Pia, wawekezaji wanaweza kuwa waangalifu kuwekeza kwenye nchi zinazokumbwa na mfumuko wa bei au mabadiliko ya haraka ya kiuchumi.
Tanzania ina mkakati gani kukabiliana na athari hizo?
Katika kukabiliana na hali hizi, serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu, katika hatua ya kihistoria, imeanza kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha uchumi unakuwa na kinga dhidi ya misukosuko ya kimataifa.
Moja ya mikakati mikubwa inayotekelezwa hivi sasa ni kuongeza akiba ya taifa ya dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania. Kupitia mkataba wa kihistoria ulioingiwa Mei 2024, Tanzania ilianza rasmi kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji na makampuni kama Geita Gold Mining kwa kutumia utaratibu wa kisheria wa ununuzi wa moja kwa moja.
Benki Kuu ya Tanzania imetangaza mpango wa kununua tani sita za dhahabu kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kama sehemu ya mpango wa kuimarisha akiba ya taifa. Tayari dhahabu zaidi ya kilo 3,600 imehifadhiwa, ikiwa ni pamoja na kilo 2,775 katika tawi la BoT Mwanza, kilo 719 Dodoma, na kilo 162 katika Benki ya England.
Lengo la mkakati huu ni kuwa na hifadhi ya thamani itakayoweza kusaidia kulinda uchumi wa taifa pale ambapo masoko ya fedha au bidhaa kama mafuta yanapokuwa na misukosuko mikubwa.
Ununuzi wa dhahabu kwa wingi utasaidia Tanzania kupunguza utegemezi wa fedha za kigeni kama dola na euro, ambazo mara nyingi hupanda thamani pindi kunapokuwa na taharuki ya kimataifa. Hifadhi ya dhahabu pia ni mali halisi isiyopoteza thamani kwa haraka, na inaweza kutumika wakati wowote kama njia ya kudhibiti mfumuko wa bei au hata kuhifadhi uwezo wa manunuzi wa taifa.
Wakati dunia ikikumbwa na changamoto za kiusalama na kisiasa kutoka Mashariki ya Kati, Tanzania imeonesha utayari wa kujilinda kwa kutumia mikakati ya kifedha inayolenga kuimarisha hifadhi ya taifa.
Kupitia hatua kama kuongeza akiba ya dhahabu na kuhimiza matumizi ya nishati mbadala kama gesi asilia, Tanzania inajitengenezea njia ya kuwa na uchumi thabiti unaoweza kustahimili misukosuko ya nje.